Tumaini Kuu

82/254

John Knox

Hamilton na Wishart, na wafuasi wao wengi na wanyenyekevu, walitoa maisha yao kuchomwa moto. Kutoka katika rundo la majivu ya kuni zilizomteketeza Wishart kwa moto, alitokea mtu mmoja ambaye asingenyamazishwa na miali ya moto, mtu mmoja aliyekuwa anaongozwa na Mungu angekuja kuukomesha utawala wa Papa nchini Scotland. TK 162.2

Alipoachana na mapokeo ya kanisa John Knox aligeukia kujilisha ukweli wa Neno la Mungu. Mafundisho ya Wishart yalithibitisha azma yake ya kulitelekeza Kanisa la Roma na kujiunga na Wanamatengenezo waliokuwa wanateswa. TK 162.3

Marafiki zake walikuwa wanamsihi kuhubiri lakini yeye alikuwa amenywea kwa sababu ya uzito wa wajibu huo. Baada ya siku zilizokuwa na mgongano wa kuhuzunisha katika nafsi yake, alikubali. Mara alipokubali alisonga mbele kwa ujasiri na bila woga wowote. Mwanamatengenezo huyu mwaminifu alikuwa haogopi uso wa mwanadamu. Alipokutana uso kwa uso na malkia wa Scotland, John Knox hakuwa mtu wa kurubuniwa kwa miPapaso ya mahaba wala hakuwa mtu wa kutetemeka kwa vitisho. Malkia alidai kuwa Knox, alikuwa amewafundisha watu kuipokea dini iliyokuwa imepigwa marufuku na serikali, na kwa hivyo alikuwa amelivunja agizo la Mungu linalowataka raia kuwatii wakuu wao. Kwa uthabiti alijibu, “Endapo wazao wote wa Ibrahimu wangekuwa wafuasi wa dini ya Farao, watu ambao walikuwa kwa muda mrefu chini ya utawala wao, ninakuuliza mheshimiwa, ni dini ya aina gani ingekuwepo duniani? Au endapo watu wote waliokuwepo wakati wa mitume wangekuwa wafuasi wa wafalme wa Rumi, ni dini aina gani ingekuwepo juu ya uso wa dunia?” TK 162.4

Mariamu alimwuliza mwanamatengenezo: “Nyie wanamatengenezo mnayafasili Maandiko Matakatifu kwa namna nyingine, na kanisa Kikatoliki nao wanayafasili kwa njia nyingine, nani nimwamini kati yenu, na ni nani atakuwa mwamuzi kwa hilo?” TK 163.1

“Inakulazimu umwamini Mungu, hilo limenenwa waziwazi katika neno lake,” alijibu Mwanamatengenezo huyo. “Neno la Mungu ni rahisi na linajifafanua lenyewe; iwapo itatokea kwa sehemu fulani fumbo au kutoeleweka, Roho Mtakatifu, ambaye hajipingi mwenyewe, hulifafanua kinagaubaga neno hilo katika sehemu nyingine za Maandiko.” 161 TK 163.2

Kwa ujasiri mkubwa Mwanamatengenezo huyu asiyeogopa chochote, kwenye hatari kubwa iliyokuwa inamkabili, alisonga mbele na kusudi lake hadi kuhakikisha Scotland imekombolewa kutoka katika utawala wa Papa. TK 163.3

Huko Uingereza kuanzishwa kwa Uprotestanti kama dini ya taifa kulikuwa kumefifia, lakini jambo hilo halikuyamaliza kabisa mateso. Nyingi kati ya desturi za Kanisa la Roma walibaki nazo. Utawala wa Papa ulikuwa umekataliwa lakini mahali pake mfalme alitawazwa kuwa kiongozi wa kanisa. Walikuwa wameucha sana usafi wa Injili. Uhuru wa dini ulikuwa bado haujaeleweka sawasawa. Ijapo unyama uliokuwa unatumiwa na Kanisa la Roma waliuacha na kwa nadra vitendo hivyo vilikuwa vinafanywa na watawala wa Kiprotestanti, bado haki ya kila mtu kumwabudu Mungu kulingana na dhamiri yake haikutambuliwa. Waliokuwa wanajaribu kumwabudu Mungu kwa namna tofauti waliendelea kuteswa kwa mamia ya miaka. TK 163.4