Tumaini Kuu

21/254

Mgunduzi wa Uovu Aliyc Makini

Wycliffe alikuwa mgunduzi makini wa uongo na alikabili bila hofu udhalilishaji uliokuwa umeshinikizwa na Kanisa la Roma. Huku akiwa kasisi wa ikulu, aliamua kusimama kidete dhidi ya malipo ya kodi iliyodaiwa na Papa kutoka kwa mtawala mkuu wa Uingereza. Papa kujitwalia mamlaka juu ya watawala wa dunia ilikuwa kinyume na haki na ufunuo. Matakwa ya Papa yalikuwa yameamsha hasira, na mafundishoya Wycliffe yalivutia mawazo ya watu muhimu katika taifa. Mfalme na wenye vyeo waliungana katika kukataa kulipa kodi. TK 54.1

Watawa maskini walirundikana Uingereza, wakiweka vizuizi katika ukuu na mafanikio ya taifa. Maisha ya watawa ya kutokuwa na kazi na ufukara yalikuwa hayanyonyi tu raslimali za watu, bali pia yalifanya kazi zilizokuwa za maana zidharaulike. Vijana walivunjwa mioyo na kuharibiwa. Wengi walishawishwa kuingia katika maisha ya utawa siyo tu bila kibali cha wazazi wao, lakini pia hata bila utashi wao, na pia ikiwa ni kinyume cha matakwa yao. Kwa kutumia “unyama huu uliopita kiasi,” kama Luther alivyoeleza baadaye, “ikiwapendeza zaidi mbwa mwitu na walio dhalimu kuliko Mkristo na mwanadamu,” mioyo ya watoto ilifanywa kuwa migumu dhidi ya wazazi wao. 8 TK 54.2

Hata wanafunzi katika vyuo vikuu walidanganywa na watawa na kushawishwa kujiunga na mfumo wao. Mara walipokuwa wanafungwa katika mtego huo ilikuwa vigumu kupata uhuru. Wazazi wengi walikataa kuwapeleka watoto wao kwenye vyuo vikuu. Shule zilidumaa, na ujinga ukatawala. TK 55.1

Papa alikuwa amewapa hawa watawa mamlaka ya kusikiliza toba na kutomsamaha-chanzo cha uovu mkubwa. Watawa, wakiwa wamedhamiria kuongeza mapato yao walikubali kabisa kutoa msamaha kiasi kwamba wahalifu waliamua kukimbilia kwao, na uovu mbaya zaidi ukaongezeka kwa kasi. Zawadi ambazo zingewasaidia wagonjwa na maskini zilipelekwa kwa watawa. Utajiri wa watawa uliendelea kuongezeka, na majumba yao ya kifahari na meza zao za anasa vilifanya ongezeko la ufukara wa taifa kuwa dhahiri zaidi. Lakini watawa hawa waliendelea kutawala fikira za umma huo wenye mapokeo potovu na wakawafanya waamini kuwa wajibu pekee wa kidini ulikuwa kuutambua ukuu wa Papa, kuabudu watakatifu, kuwapa zawadi watawa, na kwamba haya yalikuwa yanatosha kuwapatia nafasi mbinguni. TK 55.2

Wycliffe kwa kutambua vema aligonga kwenye shina halisi la uovu, akatangaza kuwa mfumo wenyewe haukuwa wa kweli na ilikuwa inapasa uondolewe. Mjadala na uchunguzi vilianza. Wengi walifanywa wajihoji kama ilikuwa muhimu kupata msamaha toka kwa Askofu wa Kanisa la Roma badala ya Mungu. (Angalia Kiambatisho.) “Watawa na makasisi wa Kanisa la Roma,” walisema, “wanatuangamiza kama saratani. Inapasa Mungu atuokoe, la sivyo watu wataangamia.” 9 Watawa hawa waliokuwa ombaomba walidai kuwa walikuwa wanafuata mfano wa Mwokozi, wakatangaza kwamba Yesu na wanafunzi wake walikuwa wanasaidiwa na hisani za watu. Dai hili lilifanya wengi waiangalie Biblia ili wajifunze wenyewe ukweli. TK 55.3

Wycliffe alianza kuandika na kuchapisha vitini kupinga watawa, akiwarejesha watu kwenye mafundisho ya Biblia na Mwandishi wake. Asingekuwa na njia bora zaidi ya hii ya kuuharibu mtego mkubwa huo ambao Papa alikuwa ameuweka, na ambao mamilioni walikuwa wamenaswa nao. TK 55.4

Wycliffe aliyekuwa ameitwa kuitetea haki za ufalme wa Uingereza dhidi ya uvamizi wa Kanisa la Roma, aliteuliwa kuwa balozi wa mfalme kule Uholanzi. Hapa alikutana na viongozi wa kanisa kutoka Ufaransa, Italia na Hispania na akapata fursa ya kuona mambo ambayo alipokuwa Uingereza yalikuwa yamefichika kwake.Ndani ya wawakilishi hawa kutoka kwenye mahakama ya Papa alielewa vema tabia halisi ya uongozi wa kanisa. Kwa shauku kubwa alirejea Uingereza ili arudie mafundisho yake ya awali, akitangaza kuwa kiburi na udanganyifu vilikuwa ni miungu ya Kanisa la Roma. TK 56.1

Baada ya Wycliffe kurudi Uingereza, aliteuliwa na mfalme kwenda kuwa paroko wa Lutterworth. Hii ilikuwa uthibitisho kwamba mfalme hakuwa amechukizwa na uwazi wa Wycliffe. Mvuto wa Wycliffe ulionekana katika kurekebisha imani katika taifa. TK 56.2

Baada ya muda mfupi hasira za Papa zilielekezwa kwake. Kutoka kwa Papa yalitolewa matamko matatu yakiamuru hatua za haraka za kumnyamazisha huyu mwalimu wa “uzushi” 10 TK 56.3

Matamko ya utawala wa Papa yaalipofika Uingereza yalisababisha Uingereza yote kuwekewa amri ya kuwafunga gerezani wazushi. (Angalia Kiambatisho.) Ilionekana dhahiri kuwa lazima baada ya muda mfupi Wycliffe angeangukia katika kisasi cha Kanisa la Roma. Lakini Yeye aliyewahi kumtamkia mtu mmoja zamani, “usiogope....mimi ni ngao yako” (Mwa. 15:1), alinyoosha mkono wake kumlinda mtumishi wake. Mauti ikaja, siyo kwa Mwana matengenezo, bali kwa Papa aliyekuwa ametoa tamko la kuangamizwa kwa Wycliffe. TK 56.4

Kifo cha Gregory XI kilifuatiwa na uchaguzi wa Mapapa wawili waliohasimiana. (Angalia Kiambatisho.) Kila mmoja aliwaambia wafuasi wake wafanye vita dhidi ya wale wa upande mwingine, akishinikiza matakwa yake kwa maapizo ya kutisha dhidi ya wapinzani wake na ahadi za thawabu kule mbinguni kwa wale wanaomuunga mkono. Makundi haya hasimu yalifanya kila yalilokuwa yanaweza kushambuliana, na Wycliffe akapumzika kwa muda. TK 56.5

Pamoja na na kusababisha mvutano na ufisadi , mpasuko huu, uliandaa njia kwa ajili ya Matengenezo kwa kuwawezesha watu kuona uhalisi wa mamlaka ya Papa. Wycliffe aliwaomba watu wachunguze kama Mapapa hawa wawili walikuwa hawasemi ukweli walipokuwa wakishutumiana kila mmoja na mwenzake kuwa ni mpinga Kristo. TK 57.1

Wycliffe akiwa ameazimu kwamba nuru ipelekwe katika kila sehemu ya Uingereza, aliandaa kundi la wahubiri, wasio na makuu, wenye kumcha Mungu, walioupenda ukweli na kuwa na shauku ya kuusambaza. Watu hawa, kwa kufundisha kwenye masoko, mitaa ya miji mikubwa, na katika njia mashambani, waliwatafuta wazee, wagonjwa na maskini, wakawafunulia habari njema za neema ya Mungu. TK 57.2

Pale Oxford, Wycliffe alihubiri Neno la Mungu kwenye kumbi za Chuo Kikuu. Akapewa sifa ya kuitwa “Daktari wa Injili.” Lakini kazi kuu kuliko zote katika maisha ya Wycliffe ilikuwa kutafsiri Maandiko kwa Kiingereza, ili kila mtu nchini Uingereza aweze kusoma matendo ya Mungu ya ajabu. TK 57.3