Tumaini Kuu

20/254

Sura Ya 5 - Nuru Yachomoza Uingereza

Mungu hakuvumilia kuona Neno lake likiangamizwa kabisa. Katika nchi mbalimbali za Ulaya watu walisukumwa na Roho wa Mungu kuutafuta ukweli kama kutafuta hazina zilizofichwa. Kwa bahati njema, kwa kuongozwa na Maandiko Matakatifu wao wenyewe walikubali kupokea nuru kwa gharama yoyote. Japokuwa hawakuweza kufahamu mambo yote, waliwezeshwa kugundua ukweli mwingi uliokuwa umefichika kwa muda mrefu. TK 53.1

Ulikuwa umefika wakati Maandiko yafikishwe kwa watu katika lugha zao za asili. Wakati wa giza nene kwa ulimwengu ulikuwa umekwisha kupita. Katika miji mingi kulikuwa na dalili za mapambazuko yaliyokuwa karibu kuja. TK 53.2

Mnamo kame ya kumi na nne, “nyota ya asubuhi ya Matengenezo” ilichomoza Uingereza. John Wycliffe alikuwa anafahamika chuoni kutokana na bidii yake katika kumcha Mungu pamoja na umahiri wake katika masomo. Alipewa elimu ya juu ya falsafa, kanuni za kanisa, na sheria za kiraia, ili kumwandaa kwa ajili ya kuingia katika pambano kubwa la uhum wa kiraia na wa kidini. Alikuwa amepata elimu ya juu ya masomo hayo, na alielewa mbinu za wasomi. Uelewa wake mpana na wa kina ulifanya aheshimiwe na marafiki na maadui zake pia. Adui zake walishindwa kudhalilisha kazi ya matengenezo kwa kuonesha ujinga au udhaifu wa aliyekuwa anaitetea. TK 53.3

Wycliffe alipokuwa bado yuko chuoni, alijiingiza katika kuchunguza Maandiko. Kabla ya hapo, alikuwa ameona hitaji kubwa, ambalo taaluma yake ya uanazuoni wala mafundisho ya kanisa havikuweza kulikidhi. Katika Neno la Mungu alipata kile ambacho alikuwa amekitafuta mahali pengine bila ya mafanikio. Humo alimwona Kristo akioneshwa kama wakili pekee kwa ajili ya mwanadamu. Akaazimu kuutangaza ukweli aliougundua. TK 53.4

Wycliffe alipokuwa anaanza kazi yake, alikuwa hajakusudia kuwa mpinzani wa Kanisa la Roma. Lakini kadiri alivyotambua makosa ya mamlaka ya Papa, ndivyo alivyozidi kudhihirisha kwa bidii zaidi mafundisho ya Biblia. Aligundua kuwa Kanisa la Roma lilikuwa limeacha Neno la Mungu kwa ajili ya mapokeo ya watu. Aliwashutumu bila hofu makasisi kwa kupiga marufuku Maandiko, na akataka Biblia irejeshwe kwa watu na mamlaka yake yaimarishwe tena kanisani. Alikuwa mhubiri hodari na mwenye lugha ya kushawishi, na maisha yake ya kila siku yalikuwa kielelezo cha ukweli aliokuwa anauhubiri. Ujuzi wake wa Maandiko, usafi wa maisha yake, ujasiri na uadilifu wake vilimpa heshima kubwa. Wengi waliona uovu katika Kanisa la Roma. Wengi bila kuficha furaha yao waliupokea kwa shangwe ukweli uliofunuliwa na Wycliffe . Lakini viongozi wa utawala wa Papa walikasirika sana; huyu mwana matengenezo alikuwa anapata umaarufu kuliko wao. TK 53.5