Tumaini Kuu

19/254

Kanisa la Roma Laazimu Kuwaangamiza Wawaldensia

Sasa vita mbaya zaidi ya kidini ilianza dhidi ya watu wa Mungu katika nyumba zao za milimani. Wapelelezi na watesaji walitumwa kuwafuatilia. Mara kwa mara mashamba yao yenye rutuba yaliharibiwa, makazi na makanisa yao madogo yaliteketezwa kabisa. Hakuna tuhuma ambayo ingeweza kuletwa dhidi ya uadilifu wa kundi hili lilokuwa limepigwa marufuku. Kosa lao kubwa lilikuwa kwamba hawakuwa tayari kumwabudu Mungu kulingana na matakwa ya Papa. Kila aina ya matusi na mateso ambayo wandamu au maShetani wangeweza kuyafikiria, yalielekezwa kwao kwa ajili ya “uhalifu” huo. TK 51.4

Kanisa la Roma Iilipoazimu kuangamiza kundi hili la kidini lililokuwa linachukiwa, tamko rasmi kutoka kwa Papa lilitolewa likiwatuhumu kuwa waasi na kuwatoa ili wanyongwe. (Angalia Kiambatisho.) Hawakuwa wanatuhumiwa kuwa wavivu, au kutokuwa waaminifu, au kwa kutofuata utaratibu; lakini ilidaiwa kuwa walikuwa na mwonekano wa utauwa na utakatifu uliokuwa unapotosha “kondoo wa kundi la kweli.” Amri hii ya Papa ilikuwa inawataka washiriki wote wa kanisa kuungana katika vita vya kidini dhidi ya “waasi” hawa. Kama motisha, amri hiyo, “iliwaondolea nadhiri zao wote waliokuwa wanajiunga na vita hiyo; iliwahalalishia umiliki wa ardhi yo yote ambayo huenda walikuwa hawakuipata kihalali, na iliwaahidi ondoleo la dhambi zao zote wale ambao wangeua mwasi ye yote. Amri hiyo ilifuta mikataba yote iliiyokuwa imefanywa kwa manufaa ya Wawaldensia, ikawazuia watu wote kuwapatia msaada wa aina yo yote, na iliwaruhusu watu wote kutwaa ardhi zao.” 7 Waraka huu unaonesha wazi kabisa kuunguruma kwa joka, na wala siyo sauti ya Kristo. Roho ile ile iliyomsulubisha Kristo na kuwaua mitume, iliyomchochea Nero mwenye uchu wa damu dhidi ya waaminifu katika wakati wake, ilikuwa inajitahidi kuwaondoa duniani wale waliokuwa wanapendwa na Mungu. TK 51.5

Licha ya kukabiliana na vita ya dini dhidi yao na ukatili wa kinyama, watu hawa waliokuwa wanamcha Mungu, waliendelea kutuma wamisionari ili waeneze ukweli huu wa thamani. Waliwindwa hadi kuuawa, na bado damu yao ilimwagilia mbegu iliyokuwa imepandwa na ikazaa matunda. TK 52.1

Hivi ndivyo, Wawaldensia walivyomshuhudia Mungu kame kadhaa kabla ya Luther. Walipanda mbegu za Matengenezo ambayo yalianza wakati wa Wycliffe, yakaendelea kukua na kuenea zaidi katika siku za Luther, na inapasa Matengenezo hayo yaendelezwe mpaka mwisho wa wakati. TK 52.2