Tumaini Kuu

18/254

Kuuvamia Ufalme wa Shetani

Wamisionari wa Kiwaldensia walikuwa wanatoa kwa tahadhari sehemu za Maandiko Matakatifu. Nuru ya ukweli ilipenya katika akili nyingi zilizokuwa zimetiwa giza, hadi Jua la Haki alipoangaza moyoni kwa uponyaji katika miali yake. Mara nyingi msikilizaji alikuwa anatamani sehemu fulani ya Biblia isomwe tena, kana kwamba anataka kujiridhisha kwamba amesikia vema. TK 50.2

Wengi walikuwa wanaona jinsi upatanisho wa mwanadamu kwa niaba ya mwenye dhambi ulivyokuwa bure. Walikuwa wanasema kwa mshangao: “Kristo ni kuhani wangu; damu yake ni dhabihu yangu; madhabahu yake ndiyo kitubio changu.” Nuru iliyowaangazia ilikuwa kubwa kiasi kwamba waliona kama wamepelekwa mbinguni. Hofu yote ya mauti iliondolewa. Sasa walikuwa wanatamani hata kwenda jela kama huko wangeweza kumheshimu Mwokozi wao. TK 50.3

Neno la Mungu lilikuwa linaletwa na kusomwa katika sehemu za siri, wakati fulani lilikuwa linasomwa kwa ajili ya roho moja, na wakati mwingine lilikuwa linasomwa kwa ajili ya kundi dogo lililokuwa linatamani nuru. Mara nyingi usiku mzima ulikuwa ukitumika kwa namna hii. Mara nyingi maneno kama haya yalikuwa yanasemwa: “Je, Mungu ataikubali sadaka yangu? Je, atanifurahia? Atanisamehe?” Jibu lilikuwa linasomwa, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Mt.l 1:28. TK 50.4

Watu hawa waliokuwa na furaha walirudi kwao kueneza ile nuru, kusimulia kwa wengine kadiri walivyokuwa wanaweza juu ya mambo mapya waliyojifunza. Walikuwa wamepata njia mpya na ya kweli! Maandiko yalikuwa yamegusa mioyo iliyokuwa inautamani ukweli. Mjumbe wa kweli alisonga mbele. Mara nyingi wasikilizaji wake walikuwa hawaulizi alikokuwa ametoka na alikokuwa anakwenda. Walikuwa wametekewa kiasi kwamba hawakuwa wanafikiria kumwuliza. “Je, anaweza kuwa alikuwa malaika kutoka mbinguni?” Walikuwa wanauliza. TK 50.5

Mara nyingi mjumbe wa kweli alikuwa amekwenda kwenye nchi nyingine au alikuwa anateseka kwenye magereza yaliyokuwa chini ya ardhi au alikuwa amekufa pale alipokuwa ameshuhudia ukweli. Lakini maneno aliyokuwa ameyaacha yalikuwa yakifanya kazi. TK 51.1

Viongozi wa utawala wa Papa waliona hatari kutokana na kazi za watu hawa wanyenyekevu waliokuwa wakisafiri huku na kule. Nuru ya ukweli ingeondoa mawingu mazito ya uongo ambayo yalikuwa yamewafunika watu; ingeelekeza mawazo yao kwa Mungu tu na matokeo yake ingeharibu ukuu wa Kanisa la Roma. TK 51.2

Watu hawa, waliokuwa wanashika imani ya kanisa la kale, walikuwa ushuhuda thabiti dhidi ya uasi wa Kanisa la Roma. Na kwa sababu hiyo, waliamsha chuki na mateso. Kukataa kwao kuacha Maandiko lilikuwa kosa ambalo Kanisa la Roma lisingeweza kulivumilia. TK 51.3