Tumaini Kuu
Hoja kwa Ajili ya Kumsaidia Mwanadamu
Mbingu yote iliona haki ya Mungu ikifunuliwa. Lusifa alikuwa amedai kwamba wanadamu wenye dhambi walikuwa mbali na wokovu. Lakini adhabu ya dhambi ilimwangukiwa yule aliye kuwa sawa na Mungu na mwanadamu alikuwa huru kuikubali haki ya Kristo na kwa toba na unyenyekevu kupata ushindi dhidi ya nguvu za Shetani. TK 311.1
Lakini haikuwa tu kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu hata Kristo akaja kufa duniani. Alikuja kuuonesha ulimwengu wote kuwa, Sheria ya Mungu haibadiliki. Kifo cha Kristo kinathibitisha kuwa haibadiliki na kinaonesha kwamba haki na rehema ni msingi wa serikali ya Mungu. Katika hukumu ya mwisho itaonekana kwamba hakuna kisingizio cha kuwepo kwa dhambi. Wakati hakimu wa dunia yote atakapomwuliza Shetani, “Kwa nini uliniasi?” mwanzilishi wa uovu hataweza kujitetea. TK 311.2
Katika kilio cha Mwokozi, “Imekwisha”, kengele ya kifo cha Shetani iligongwa. Pambano kuu lilikuwa limeamuliwa, kung’olewa milele kwa uovu kulikuwa ni hakika. Wakati ambapo, “siku ile inakuja, inawaka kama tanuru... wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi.” (Malaki 4:1). TK 311.3
Uovu hautaonekana tena. Sheria ya Mungu itaheshimiwa kama sheria ya uhuru. Uumbaji uliojaribiwa na kuthibitishwa hautageuka tena na kuacha utii kwake ambaye tabia yake imeonekana ni ya upendo na ana hekima isiyo na kikomo. TK 311.4