Tumaini Kuu

192/254

Sura Ya 30 - Shetani Na Mwanadamu Vitani

“Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.” (Mwanzo 3:15) Uadui huu si wa asili. Mwanadamu alipoiasi sheria ya Mungu, asili yake ikawa uovu, ikipatana na Shetani. Malaika walioanguka na wanadamu waovu walifanya muungano wa uasi. Kama Mungu asingeingilia kati, Shetani na mwanadamu wangeungana wawe kinyume na mbingu, na familia yote ya wanadamu ingekuwa imeungana kwa ajili ya kumpinga Mungu. TK 312.1

Shetani aliposikia kuwa kungekuwa na uadui kati yake na mwanamke, na kati ya uzao wake na ule wa mwanamke, alijua kuwa kwa namna fulani mwanadamu angewezeshwa kumletea upinzani. TK 312.2

Kristo anapandikiza ndani ya mwanadamu uadui dhidi ya Shetani. Pasipo hii neema ibadilishayo na nguvu ifanyayo upya, mwanadamu angeendelea daima kuwa mtumwa, tayari kumtii Shetani. Lakini kanuni hii mpya inaleta mgongano ndani ya nafsi; nguvu aitoayo Kristo inamwezesha mwanadamu kumpinga mdhalimu. Kuichukia dhambi badala ya kuipenda kunaonesha kanuni kamili ya mbinguni. TK 312.3

Uhasama kati ya Shetani na Kristo ulionekana wazi zaidi katika namna ulimwengu ulivyompokea Yesu. Usafi na utakatifu Wakristo uliamsha chuki ya waovu dhidi yake. Hali yake ya kujikana nafsi ilikuwa ni shutuma ya kudumu kwa watu wenye kiburi na wapenda anasa. Shetani pamoja na watu waovu waliungana dhidi ya mtetezi wa ukweli. Uadui ule ule unaonekana dhidi ya wafuasi Wakristo. Yeyote alipingaye jaribu ataamsha ghadhabu ya Shetani. Kristo na Shetani hawawezi kupatana. “Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa.” (2Timotheo 3:12) TK 312.4

Mawakala wa Shetani wanatafuta kuwadanganya wafuasi Wakristo na kuwashawishi wasimtii. Wanapotosha Maandiko ili kufanikisha lengo lao. Yule roho aliyemuua Yesu anawasukuma waovu kuwaangamiza wafuasi wake. Haya yote yalitabiriwa kabla katika ule unabii wakwanza usemao, “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake” TK 312.5

Ni kwa nini Shetani hapati upinzani mkubwa? Kwa sababu askari Wakristo wana muunganiko kidogo mno ulio halisi na Yesu. Kwao dhambi siyo kitu kibaya kama ilivyokuwa kwa Bwana wao. Hawana jitihada ya kuipinga. Wamepofushwa juu ya tabia ya mkuu wa giza. Watu wengi hawajui kuwa adui yao ni kamanda mkubwa apiganaye vita na Kristo. Hata wahubiri wa Injili wanadharau ushahidi wa kazi zake. Wanaonekana kuupuuzia uwepo wake. TK 313.1