Tumaini Kuu
Kufukuzwa Kutoka Mbinguni
Shetani na jeshi lake walimtupia Kristo lawama za uasi wao; kwamba kama wasingeshutumiwa wasingeasi. Wakiwa na kiburi na ufidhuli na bado kwa kufuru wakidai hawana hatia na walikuwa wameonewa na utawala wa kidikteta; mwasi mkuu pamoja na waliomwunga mkono walifukuzwa kutoka mbinguni. (Angalia Ufunuo 12:7-9). TK 309.4
Roho ya Shetani bado inaongoza uasi duniani ndani ya watoto wa kuasi. Kama alivyofanya yeye wanawaahidi watu uhuru utakaopatikana kwa kuvunja sheria ya Mungu. Shutuma dhidi ya dhambi bado huamsha chuki. Shetani anawaongoza watu kujihesabia haki wenyewe na kutafuta kuungwa mkono na wengine katika dhambi zao. Badala ya kurekebisha makosa yao, wao huchochea chuki dhidi ya mtu anayeishutumu dhambi, kana kwamba ndiye aliyesababisha shida. TK 310.1
Kwa upotoshaji ule ule wa tabia ya Mungu alioufanya mbinguni na kusababisha Mungu aonekane kuwa mkali na dikteta; Shetani alisababisha mwanadamu kutenda dhambi. Alitangaza kuwa makatazo ya Mungu yasiyo ya haki yalimfanya mwanadamu aanguke, kama yalivyomwongoza yeye kwenye uasi. TK 310.2
Kwa kumfukuza Shetani kutoka mbinguni, Mungu aliitangaza haki na heshima yake. Lakini mwanadamu alipotenda dhambi, Mungu alitoa uthibitisho wa pendo lake kwa kumtoa Mwanawe afe kwa ajili ya wanadamu walioanguka. Katika upatanisho tabia ya Mungu imefunuliwa. Hoja yenye nguvu ya msalaba huonesha kwamba serikali ya Mungu kwa namna yoyote ile haikusababisha dhambi kuwepo. Wakati wa huduma ya Mwokozi duniani, mdanganyifu mkuu alifunuliwa. Kufuru za makusudi za kumtaka Yesu amwabudu, kwa nia mbaya akimwinda kila mahali, na kuisukuma mioyo ya makuhani na watu ili wakatae upendo wake na kulia, “Msulibishe! Msulibishe!”-haya yote yalichochea bumbuwazi na uchungu kwa ulimwengu. Mkuu wa giza alitumia ujanja na nguvu zake zote ili kumwangamiza Yesu. Shetani aliajiri watu kama mawakala wake kuyajaza uchungu na mateso maisha ya Mwokozi. Moto wa wivu na kijicho, chuki na kisasi uliripuka pale Kalvari dhidi ya Mwana wa Mungu. TK 310.3
Na sasa, hatia ya Shetani ilidhihirika bila udhuru. Alikuwa ameifunua tabia yake halisi. Madai yake ya uongo dhidi ya tabia ya Mungu yalionekana katika nuru yake halisi. Alimtuhumu Mungu kwa kuwa anajiinua mwenyewe anapotaka kupokea utii kutoka kwa viumbe wake na alitangaza kuwa wakati Mwumbaji alikuwa anawahimiza wengine kujikana nafsi, Yeye mwenyewe hakujikana nafsi wala kutoa kafara yoyote. Sasa ilikuwa inaonekana kwamba Mtawala wa ulimwengu alikuwa ameitoa kafara iliyo kuu ambayo upendo ungeweza kutoa, kwani, “Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake “(2Wakonntho 5:19.) Kwa lengo la kuiangamiza dhambi Kristo alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti. TK 310.4