Tumaini Kuu

189/254

Chuki Yakomaa na kuwa llasi Halisi

Mungu kwa hekima yake alimruhusu Shetani kuendelea na kazi yake, hadi ile roho ya chuki ilipopevuka na kuwa uasi. Ilikuwa ni lazima mipango yake ifunuliwe kwa ukamilifu, ili asili yake halisi ionekane kwa wote. Lusifa alipendwa sana na viumbe mbinguni, na mvuto wake juu yao ulikuwa mkubwa. Serikali ya Mungu haikujumuisha tu wakazi wa mbinguni, bali ulimwengu wote aliokuwa ameuumba; na Shetani alipanga kuwa endapo angewachukua malaika pamoja naye katika uasi, angeweza pia kuuchukua ulimwengu wote. Akitumia hila na udanganyifu, uwezo wake wa kuhadaa ulikuwa mkubwa sana. Hata malaika waaminifu hawakuweza kuitambua tabia yake kwa ukamilifu ama kuona ni wapi kazi yake ilikuwa inaelekea. TK 308.1

Shetani alikuwa anaheshimiwa sana, na matendo yake yote yalikuwa yamesitiriwa kwa usiri, kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu kuifunua asili ya kazi yake kwa malaika. Kabla ya haijafunuliwa kwa ukamilifu; dhambi haingeonekana kuwa kitu kibaya kama ilivyokuwa. Viumbe watakatifu, hawakuweza kutambua matokeo ya kuiweka kando sheria ya Mungu. Mwanzoni Shetani alidai kwamba alikuwa akikuza heshima ya Mungu na mema ya wakazi wote wa Mbinguni. TK 308.2

Katika kushughulikia dhambi, Mungu alikuwa anatumia haki na kweli pekee. Shetani alikuwa anatumia kile ambacho Mungu hangeweza kukitumia- ubembe na ulaghai. Tabia ya kweli ya mnyang’anyi ni lazima ifahamike kwa wote. Alitakiwa apate muda wa kujifunua mwenyewe kwa kazi zake mbovu. TK 308.3

Shetani alimlaumu Mungu kwa kukosekana kwa maelewano kulikosababishwa na mwelekeo wake kule mbinguni. Alitangaza kuwa uovu wote ni matokeo ya utawala wa Mungu. Na hivyo ilikuwa lazima aoneshe utendaji wa mabadiliko aliyoyapendekeza ndani ya sheria ya Mungu. Kazi yake ni lazima imhukumu mwenyewe. Ulimwengu mzima ni lazima uone mdanganyifu akifunuliwa. TK 308.4

Hata wakati ilipoamuliwa kwamba hangeendelea kubakia mbinguni, Mungu hakumwangamiza Shetani. Utii wa viumbe wa Mungu ni uthibitisho wa haki yake. Kwa vile wakazi wa mbinguni na ulimwengu wote, hawakutayarishwa kufahamu matokeo ya dhambi, hawangeweza wakati ule, kuiona haki na rehema ya Mungu katika kumwangamiza Shetani. Endapo mara moja angefutwa asiwepo, wangekuwa wanamtumikia Mungu kwa hofu na siyo kwa upendo. Mvuto wa mdanganyifu ungekuwa haujaangamizwa kikamilifu, na wala roho ya uasi haingekuwa imeng’olewa. Kwa faida ya ulimwengu katika vizazi vyote ilikuwa ni lazima Shetani akuze kwa ukamilifu zaidi kanuni zake, ili madai yake dhidi ya serikali ya Mungu yapate kuonekana na viumbe vyote katika nuru halisi. TK 309.1

Uasi wa Shetani ulitakiwa kuwa ushuhuda kwa ulimwengu juu ya matokeo ya kutisha ya dhambi. Utawala wake ungeonesha matunda yatokanayo na kuiacha kando sheria ya Mungu. Historia ya jaribio hili la kutisha la uasi ingekuwa ni ulinzi endelevu kuwaokoa katika dhambi na adhabu yake. TK 309.2

Ilipotangazwa kwamba mnyang’anyi mkuu pamoja na wote waliomwunga mkono ni lazima wafukuzwe kutoka kwenye makao ya furaha, kiongozi wa uasi kwa ujasiri aliapa kuitweza sheria ya Mungu. Alizishutumu sheria za Mungu kwamba zinanyima uhuru na akatangaza kusudi lake la kuifuta sheria. Alisema kuwa yakiwa yameachwa huru dhidi ya kizuizi hiki; majeshi ya mbinguni yangeweza kuishi maisha yaliyotukuka zaidi. TK 309.3