Kutayarisha Njia
Shauri la Wazazi Wamchao Mungu
Pakiwako na matokeo mabaya ya ndoa namna hii, kwa nini vijana wasierevuke? Kwa nini waendelee kuona kuwa hawahitaji shauri la wazee na la watu wenye akili zaidi? Kazini, wanaume na wanawake vile vile hujihadhari sana. Kabla ya kushika kazi yo yote ya maana, wanajitayarisha kwa kazi yao. Wakati, fedha, na kujifunza sana kwa uangalifu hutumiwa kwa jambo hili, wasije wakashindwa kufaulu katika jambo wanalojaribu kufanya. KN 134.5
Basi, ni uangalifu mkubwa namna gani ungepasa kutumiwa katika kuingia ndoa-wajibu ambao unayo matokeo katika vizazi vya baadaye na kwenye maisha ya wakati ujao? Badala ya kufanya hivi, inaingiliwa kwa ubishi, bila kicho, kwa tamaa mbaya, upofu, bila kufikiri kwanza. Maelezo tu ya jambo hili ni ya kwamba Shetani hupenda kuona hali mbaya na uharibifu ulimwenguni, naye husokota wavu huu kuzitega roho za watu. Hufurahia kuwapata watu hawa walio wapumbavu kupotewa na furaha yao ya ulimwenguni humu na makao yao katika ulimwengu ujao. KN 134.6
Je, watoto wafuate mapenzi na tamaa yao wenyewe bila kujali shauri na maamuzi ya wazazi wao? Wengine kamwe hawaelekei kufikiri hata kidogo vile wazazi wao watakavyo, wala kujali maamuzi yao yaliyo ya utu mzima. Kushika lao bila kujali wengine kumeufungia mlango upendo wa baba na mama usiingie mioyoni mwao. Mioyo ya vijana yahitaji kuamshwa katika jambo hili. Amri ya tano ndiyo amri tu ambavo imeungana na ahadi, lakini inadharauliwa hata hajaliwi kabisa na dai la mchumba. Kuudharau upendo wa mama, kutoheshimu malezi ya baba ni dhambi zinazokaa hali ya kuandikwa kitabuni juu ya vijana wengi. KN 135.1
Mojawapo ya makosa makubwa kwa jambo hili ni ya kuwa vijana na wale wasio na maarifa hawataki mapenzi yao kupingwa, ya kuwa pasiwepo na cho chote kinachoyaingilia mambo ya upendo wao. Kama kuna jambo moja lenye kuhitaji kutazamwa pande zote, hili ndilo jambo hilo. Msaada wa maarifa waliyo nayo watu wengine, na kulifikiri kwa makini jambo hili pande zake zote ni muhimu kabisa. Ni jambo linalodharauliwa mno na watu wengi. Kubalini shauri la Mungu na la wazazi wenu wenye kumcna Mungu, vijana rafiki zangu. Mwombeni Mungu juu ya neno hili. KN 135.2
Pengine utauliza, “Wazazi wangechagua mchumba bila kujali moyo au maoni ya mwana au binti yao?” Nakuuliza swali kama ipasavyo: je, mwana au binti angepaswa kujichagulia mchumba bila kushauriana na wazazi, hali hatua ya namna hii haina budi kuwa na matokeo ya baadaye kuihusu furaha ya wazazi wakiwa wanapenda watoto wao? Tena ingempasa yule mtoto, bila kuiali shauri na maonyo ya wazazi wake, kuendelea bila kubadilika? Najibu kwa dhati ya moyo: La; sivyo kama haoi, Amri ya tano yakataza mwenendo wa namna hiyo. “Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.” Hii ni amri yenye ahadi ambayo Mungu hakika ataitimiza kwa wale wanaotii. Wazazi wenye busara kamwe hawatawachagulia watoto wao wachumba bila kuyajali mapenzi yao. KN 135.3
Baba na mama wangeona kuwa ni wajibu kuongoza upendo wa vijana, kusudi wapate kuwekwa kwa wale watakaokuwa wenzi wanaofaa. Wangeona kuwa ni wajibu unaowapasa, kwa mafundisho na kielelezo cha maisha yao wenyewe, kwa msaada wa neema ya Mungu, kukuza tabia ya watoto tokea utotoni mwao ipate kuwa safi na bora na wavutwe kwa wema na uadilifu. Wanaofanana huvutana; wanaofanana huthaminiana. Hebu upendo kwa neno la kweli na usafi na wema utiwe moyoni, na vijana watatafuta urafiki wa wale wenye tabia hizi. KN 135.4