Tumaini Kuu
Sura Ya 15 - Enzi Ya Hofu Kuu Ufaransa: Chimbuko Lake Halisi
Baadhi ya nchi zilikaribisha imani ya Matengenezo kama mjumbe wa Mbinguni. Katika nchi nyingine nuru ya ujuzi wa Biblia kwa ujumla ilikuwa kana kwamba imewekwa kando. Kwenye nchi moja ukweli na udanganyifu vilishindana kwa kame nyingi. Hatimaye ukweli wa mbinguni ulitupwa nje. Roho wa Mungu aliondolewa kutoka kwa watu waliokuwa wameidharau karama ya neema ya Mungu. Ulimwengu wote ulishuhudia tunda la kuikataa nuru kwa makusudi. TK 172.1
Vita dhidi ya Biblia nchini Ufaransa viliishia kwenye Mapinduzi, matokeo halali ya ukandamizaji wa Maandiko Matakatifu uliokuwa unafanywa na Kanisa la Roma.(Angalia Kiambatisho.) Jambo hili lilitoa kielelezo kikubwa cha matokeo ya mafundisho ya Kanisa la Roma kuliko vyote vilivyowahi kushuhudiwa. TK 172.2
Mwandishi wa Ufunuo anaonesha matokeo ya kuogofya ya utawala wa “mtu wa dhambi” yaliyokuwa yanarundikana huko Ufaransa: “...Nao wataukanyaga mji mtakatifu miezi arobaini na miwili. Nami nitawamhusu mashahidi wangu wawili, nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini, hali wamevikwa magunia. ...Hata watakapoumaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika kuzimu atafanya vita nao, naye atawashinda na kuwaua. Na mizoga yao itakuwa katika njia ya mji ule mkuu, uitwao kwa jinsi ya roho Sodoma, na Misri, tena ni hapo Bwana wao aliposulubiwa.... Nao wakaao juu ya nchi watafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi. Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama ju ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama.” Ufunuo 11:2-11. TK 172.3
“Miezi arobaini na miwili” na “siku elfu moja mia mbili na sitini” ni kitu kile kile, wakati ambao Kanisa la Kristo lingepata mateso kutokana na ukandamizaji wa Kanisa la Roma. Miaka 1260 ilianza mnamo mwaka 538 na kuishia mwaka 1798 B.K.(Tazama Kiambatisho.) Wakati huo jeshi la Ufaransa lilimtia nguvuni Papa, na alifia uhamishoni. Tangu wakati huo utawala wa Papa haujapata mamlaka uliokuwa nayo hapo kabla. TK 172.4
Mateso kwa Kanisa hayakuendelea kwa miaka yote 1260. Rehema ya Mungu ilipunguza muda huo wa mateso makali kwa watu wake yaliyokuwa yanachochewa na imani ya Matengenezo. TK 173.1
“Mashahidi wawili” wanawakilisha Maandiko Matakatifu yaani Agano la Kale na Agano Jipya, ushahidi muhimu wa chimbuko na umilele wa sheria ya Mungu, na mpango wa wokovu. TK 173.2
“...Nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini, hali wamevikwa magunia.” Biblia ilipopigwa marufuku, na shuhuda zake kupotoshwa, wakati wale waliodiriki kuzitangaza kweli zake waliposalitiwa, kuteswa na kuuawa kwa sababu ya imani yao ama kulazimishwa kukimbia- “mashahidi” waaminifu walikuwa wanatoa unabii wakiwa “wamevaa nguo za magunia.” Kwenye nyakati za giza kuu wanadamu waliokuwa waaminifu walipewa mamlaka na busara kuutangaza ukweli wa Mungu. (AngaIia Kiambatisho.) TK 173.3
“Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka kwenye vinywa vyao na kuwala adui zao.” Ufunuo 11:5. Watu hawawezi kukanyaga Neno la Mungu bila kuadhibiwa! TK 173.4
“Hata watakapoumaliza ushuhuda wao.” Walipokaribia kumaliza kazi yao katika mazingira magumu, watashambuliwa na “yule mnyama atokaye katika kuzimu.” Hapa inafunuliwa upya mamlaka ya kishetani. TK 173.5
Imekuwa ni sera ya Kanisa la Roma, kudai kuwa linaiheshimu Biblia, kwa kuifungia katika lugha isiyofahamika, na kuificha watu wasiisome. Chini ya utawala wake mashahidi walikuwa wanatoa unabii “hali wamevikwa magunia.” Lakini “mnyama atokaye kuzimu.” angekiri waziwazi kupiga vita Neno la Mungu. TK 173.6
“Mji mkuu” ambamo mashahidi waliuawa kwenye mitaa yake na mizoga yao kutupwa humo ni Misri ya “kiroho.” Mataifa yote katika historia ya Biblia, ni Misri peke yake waliokataa kwa ujasiri mkubwa uwepo wa Mungu na walikuwa wanapinga maagizo Yake. Hakuna mfalme aliyediriki kufanya uasi kwa kiburi dhidi ya Mbingu kama alivyofanya Farao mfalme wa Misri: “...Mimi simjui BWANA, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao.”Kutoka 5:2. Huu ni ukanamungu; na taifa linalowakilishwa na Misri litatoa sauti ya kumkataa Mungu na kudhihirisha roho ya ujeuri. TK 173.7
“Mji mkuu” pia unalinganishwa “kiroho” na Sodoma. Ufisadi wa Sodoma ulidhihirishwa hasa katika uasherati. Dhambi hii pia ingeandamana na taifa ambalo lingetimiza andiko hili. TK 174.1
Kulingana na andiko hili la nabii, muda mfupi kabla ya mwaka 1798 mamlaka fulani zenye tabia ya kishetani zingeinuka kuipiga vita Biblia. Na kwenye nchi ambayo ushuhuda wa “mashahidi wawili” wa Mungu utanyamazishwa hivyo utabainishwa ukanamungu wa Kifarao na ufuska wa Sodoma. TK 174.2