Tumaini Kuu

23/254

Wycliffe Akataa Kukanusha

Lakini Wycliffe hakukanusha kauli yake. Alidumisha mafundisho yake, bila hofu na kukataa mashtaka ya watesi wake. Aliitisha wasikilizaji wake waje mbele ya mahakama ya kimbingu na kupima maneno yao ya hila na udanganyifu katika vipimo vya ukweli wa milele. Nguvu ya Roho Mtakatifu ilikuwa kati ya wasikilizaji. Kama mishale itokayo katika podo la Bwana, maneno ya Mwanamatengenezo yalipenya mioyoni mwao. Akawageuzia shitaka la uzushi, ambalo walikuwa wameliweka dhidi yake. TK 59.3

Alisema, “Je, mnadhani mnapambana na nani? Mzee anayekaribia kaburi? La! na Ukweli-Ukweli ulio na nguvu kuliko ninyi, na utawashinda.” 12 Baada ya kusema hivyo, aliondoka na hakuna hata mmoja kati ya adui zake waliojaribu kumzuia. TK 59.4

Kazi ya Wycliffe ilikuwa imekaribia kuisha, lakini kwa mara nyingine tena alikuwa atoa ushuhuda kwa ajili ya Injili. Aliitwa kwa ajili ya shitaka mbele za mahakama ya utawala wa Papa pale Roma, ambayo mara nyingi ilimwaga damu ya watakatifu. Mshtuko uliopelekea kupooza ulifanya isiwezekane kwake kufanya safari hiyo. Lakini, ingawa sauti yake haingesikika Roma, angeweza kunena kwa njia ya maandishi. Mwanamatengenezo alimwandikia Papa barua, ambayo, ikionesha heshima na roho ya Ukristo, ilikuwa kemeo kali kwa ufahari na kiburi cha mamlaka ya Papa. TK 60.1

Wycliffe aliwasilisha kwa Papa na makadinali upole na unyenyekevu Wakristo, akionesha siyo tu kwao, bali pia kwa jumuiya yote ya Kikristo, tofauti kati yao na Mkuu ambaye walidai kumwakilisha. TK 60.2

Wycliffe alitegemea kikamilifu kwamba uhai wake ulngekuwa malipo kwa uthabiti wake. Mfalme, Papa na maaskofu waliungana ili kukamilisha maangamizi yake, na ilielekea kuwa isingechukuwa miezi mingi hadi yeye kufikishwa hatua ya kuchomwa moto. Lakini ujasiri wake haukutikisika. TK 60.3

Mtu ambaye katika maisha yake yote alikuwa amesimama imara akitetea ukweli, hangepaswa kuwa mhanga wa hasira ya adui zake. Bwana alikuwa mlinzi wake; na sasa, wakati adui zake walipojisikia kuwa na hakika ya kupata windo lao, mkono wa Mungu ulimwondoa kutoka katika upeo wao. Akiwa kanisani kwake pale Lutterworth, hali akiwa tayari kuongoza katika huduma ya chakula cha Bwana, alipooza na kuanguka, na katika muda mfupi akakata roho. TK 60.4