Tumaini Kuu

123/254

“Wakati Umetimia”

Kristo aliwatuma wakiwa na ujumbe: “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.” Marko 1:15. Ujumbe huo ulikuwa unatokana na unabii wa Danieli 9. “Majuma sitini na tisa” yalikuwa yaishie kwa “Masihi mkuu,” nao wanafunzi kwa shauku kuu walikuwa wanatazamia kuanzishwa kwa ufalme wa Masihi huko Yerusalemu, ili atawale ulimwengu mzima. TK 220.1

Walihubiri ujumbe uliokabidhiwa kwao, ingawa hawakuelewa maana yake. Wakati ujumbe wao ulikuwa unatokana na Danieli 9:25, hawakuona katika aya inayofuata kuwa Masihi angekatiliwa mbali. Mioyo yao ilikuwa ikifikiria utukufu wa enzi ya kidunia; jambo hilo lilipofusha ufahamu wao. Katika muda ule ule waliokuwa wanatarajia kumwona Bwana wao akikalia kiti cha enzi cha Daudi, walimwona akikamatwa, na kupigwa, na kudhihakiwa, na kuhukumiwa kifo cha msalaba. Mioyo ya wale wanafunzi iliumia sana kwa fadhaa na uchungu mkubwa! TK 220.2

Kristo alikuwa katika wakati ule uliokuwa umetabiriwa. Maandiko yalikuwa yametimia katika kila kipengele. Neno na Roho wa Mungu walikuwa wanashuhudia kazi ya kimbingu ya Mwana wake. Lakini akili za wanafunzi zilikuwa zimegubikwa na mashaka. Ikiwa kweli Yesu alikuwa Masihi, wangetumbukiaje kwenye huzuni na kuvunjika kwa matumaini yao? Hili ndilo swali lililokuwa linawasumbua nafsi wakati walipokuwa wamekata tamaa siku ile ya Sabato iliyokuwa katikati ya kifo na kufufiika kwake. TK 220.3

Hata hivyo walikuwa hawajaachwa. “Nikaapo gizani, BWANA atakuwa nuru yangu... Atanileta nje kwenye nuru, nami nitaiona haki yake.” “Nuru huwazukia wenye adili gizani.” “Nitafanya giza kuwa nuru mbele yao; na mahali palipopotoka kuwa pamenyoka. Haya nitayatenda, wala sitawaacha.” Mika 7:8,9; Zaburi 112:4; Isaya 42:16. TK 220.4

Tangazo lililofanywa na wanafunzi lilikuwa sahihi, “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia.” Mwisho wa ule muda wa majuma sitini na tisa wa Danieli 9, ungeishia kwa Masihi, yaani “Mtiwa Mafuta”—Kristo alitiwa mafuta na Roho Mtakatifu baada ya kubatizwa na Yohana. “Ufalme wa Mungu” haukuwa wa ulimwengu huu, kama walivyokuwa wamefundishwa kuamini. Wala haukuwa ule ufalme ujao usiokuwa na mwisho, ambapo “wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii.” (Danieli 7:27). TK 221.1

Usemi huu “ufalme wa Mungu” unamaanisha ufalme wa neema na ufalme wa utukufu. Mtume Paulo anasema: “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.” Waebrania 4:16. Kuwepo kwa kiti cha enzi kunamaanisha kuwepo kwa ufalme. Kristo anatumia usemi huu “ufalme wa mbinguni” kuelezea kazi ya neema katika mioyo ya watu. Hivyo kiti cha utukufu kinawakilisha ufalme wa utukufu. Mathayo 25:31, 32. Ufalme huu ni wa baadaye. Hautasimamishwa hadi hapo Kristo atakapokuja mara ya pili. TK 221.2

Wakati Kristo alipoutoa uhai wake na kupaza sauti, “Imekwisha,” ahadi ya wokovu, iliyokuwa imetolewa kwa wale wanandoa wawili wenye dhambi katika bustani ya Edeni, ilithibitishwa. Ufalme wa neema, ambao ulikuwa upo kwa ahadi ya Mungu, sasa ulisimamishwa. TK 221.3

Kwa hiyo, kifo cha Kristo—tukio ambalo wanafunzi waliona kama uangamivu wa tumaini lao—ndicho kiichofanya tumaini hili liwe la uhakika milele. Japo liliwavunja moyo kabisa, lilikuwa uthibitisho kuwa kuamini kwao kulikuwa sahihi. Tukio ambalo liliwavunja moyo lilikuwa linafungua mlango wa matumaini kwa waaminifu wote wa Mungu katika vizazi vyote. TK 221.4

Dhahabu safi ya upendo wa wanafunzi kwa Yesu ilikuwa imechanganyika na hali duni za nia zenye ubinafsi. Dira yao ilikuwa ni kiti cha enzi, taji, na utukufu. Kiburi cha moyo, tamaa ya fahari za kidunia, iliwafanya wasizingatie maneno ya Mwokozi yaliyokuwa yanaonesha ufalme wake ulivyo, yakielekeza kwenye mauti yake. Makosa hayo yalisababisha majaribu ambayo yaliruhusiwa kwa ajili ya kuwarudi. Injili tukufu ya Bwana aliyefufuka ilikuwa ikabidhiwe kwa wanafunzi hao. Tukio lililoonekana kuwa la uchungu sana liliruhusiwa ili kuwaandaa kwa ajili ya kazi hiyo. TK 221.5

Baada ya kufufuka kwake, Yesu aliwatokea wanafunzi wake katika njia ya kwenda Emau, “akawaeieza katika Maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.” Lengo lake lilikuwa kukuza imani yao juu ya “lile neno la unabii lililo imara zaidi” (Luka 24:27; 2 Petro 1:19), si kwa ushuhuda tu, bali kwa unabii wa Agano la Kale. Na kama hatua ya kwanza kabisa ya kuwapatia maarifa hayo, Yesu aliwaelekeza wanafunzi wake katika vitabu vya “Musa na manabii wote” wa Maandiko ya Agano la Kale. TK 222.1