Tumaini Kuu
Kile Ambacho Kingetokea
“Kukimbia kwa jamii ya Hugenots kulisababisha kudhoofika kwa Ufaransa katika hali zote. Miji ya viwanda iliyokuwa kwenye hatua za ustawi ilianguka na kuchakaa.... Inakisiwa kwamba mwanzoni mwa siku za Mapinduzi, kulikuwa na ombaomba wapatao mia mbili elfu katika mji wa Paris waliokuwa wanaomba msaada kutoka mikononi mwa mfalme. Kwenye taifa hili lililokuwa linaendelea kudhoofika ni Majesuti peke yao ndio waliokuwa wamestawi.” 179 TK 180.3
Injili ingeleta suluhisho kwa matatizo yaliyokuwa yanaisumbua Ufaransa na kuwatatiza viongozi wake wa kidini, mfalme, na wabunge, ambayo hatimaye yalilitumbukiza taifa hili kwenye uharibifu. Chini ya uongozi wa Kanisa la Roma watu walikuwa wamepoteza mafundisho ya Mwokozi ya kujikana nafsi na upendo usio na ubinafsi kwa kuwatendea mema watu wengine. Matajiri hawakukemewa kwa kuwagandamiza maskini wala maskini hawakuwa na msaada katika hali yao duni. Ubinafsi wa wenye mali na wenye nguvu ulikuwa umezidisha unyanyasaji. Kwa kame nyingi, matajiri walikuwa wanawakosea maskini na maskini waliwachukia matajiri. TK 181.1
Katika majimbo mengi wafanyakazi walikuwa wanategemea huruma za wenye mali na walilazimishwa kutekeleza matakwa makubwa kupita kiasi. Watu wa daraja la kati na la chini walikuwa wanatozwa kodi kubwa na mamlaka za serikali na mapadre. “Wakulima na wakulima wadogo walikuwa wanakufa bila bwana huyu mdhalimu kujali... Maisha ya wafanyakazi mashambani yalikuwa yenye kazi zisizokoma, na taabu isiyo na kupumzika; malalamiko yao ... yalipuuzwa na walikuwa wanatendewa jeuri.... Majaji walikuwa wanapokea rushwa waziwazi...Chini ya nusu ya kodi iliyokuwa inatozwa ilifika katika hazina ya mfalme au hazina ya askofu; sehemu iliyobaki ilikuwa inatumiwa vibaya na kutapanywa kwenye mambo ya anasa. Watu waliowafukarisha wenzao kiasi hicho walikuwa wamesamehewa kulipa kodi na walikuwa wameruhusiwa kisheria au na desturi pia kuwekwa katika vyeo vyote vilivyokuwepo serikalini.... Kwa kutimiza tamaa zao mamilioni walizamishwa kwenye maisha duni na yasiyokuwa na matumaini. (Angalia Kiambatisho.) TK 181.2
Kwa zaidi ya nusu kame kabla ya Mapinduzi ya Ufaransa, nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Louis XV, mfalme huyu alijulikana kwa uzembe, kutokuwa makini, na uasherati. Na huku hazina ya nchi ikiwa imefilisika na watu wamekasirishwa vilivyo, halikuhitajika jicho na nabii kuona matokeo ya kutisha yaliyokuwa mbele. Hitaji la marekebisho lilikuwa linasisitizwa bila mafanikio. Maangamizi yaliyokuwa yanaikabili Ufaransa yalionekana katika jibu la ubinafsi na lenye fumbo la mfalme, “Baada yangu ni mafuriko!” TK 181.3
Kanisa la Roma lilikuwa limewafundisha wafalme na watawala kuwafanya watu kuwa watumwa, likikusudia kuwafunga pingu mioyoni mwao viongozi na watu wa kawaida. Mambo mengi ya kutisha kuliko maumivu ya kimwili yaliyosababishwa na sera za Kanisa la Roma ilikuwa ni mmomonyoko mkubwa wa maadili. Wakiwa wamenyimwa Biblia na kuachwa kuishi maisha ya ubinafsi, watu walikuwa wamegubikwa na ujinga na kuzama kwenye maovu, na hawakuwa wanafaa kutawala nafsi zao. TK 182.1