Kutayarisha Njia
Sura Ya 19 - Kutooana na Mtu Asiyeamini
MIONGONI mwa Wakristo kuna dharau na kutojali mafundisho ya Neno la Mungu; Hali ambayo ni ya kustaajabisha na kutia hofu juu ya ndoa ya Wakristo kuoana na makafiri. Wengi wanaojidai kumpenda na kumcha Mungu huchagua kufuata maelekeo ya mioyo yao wenyewe badala ya kukubali shauri la Mungu. Katika jambo ambalo linahusu kabisa raha na hali njema ya sehemu zote mbili kwa ulimwengu huu na kwa ule ujao, akili, busara, na kicho cha Mungu huwekwa kando; na tamaa mbaya ya kuharikisha, ukaidi huachwa kutawala. KN 139.1
Wanaume kwa wanawake ambao wangekuwa wenye akili na bidii ya kufanya vizuri mambo yote yawapasayo, huziba masikio yao wasisikie shauri jema; ni viziwi wasiosikia maombi na maonyo ya rafiki na jamaa wala ya watumishi wa Mungu. Maneno ya shauri ama onyo huhesabiwa kama ufidhuli, na rafiki anayekuwa mwaminifu hata kuthubutu kusema onyo hutendwa kama adui. Haya yote ndivyo Shetani apendavyo. Hufuma mtego wake kuizunguka roho ya mtu, naye hupotewa na akili, na kupumbazika. Akili hushindwa kujitawala na tamaa mbaya hutamalaki; ashiki hutawala, mpaka mtu akaamka akiwa amekwisha kuchelewa sana na kuwa katika maisha ya hali mbaya ya taabu na utumwa. Haya si mambo ya kuwaziwa tu, bali ni maneno ya kweli. Kibali cha Mungu hakitolewi kwa umoja ambao ameukataza wazi. KN 139.2
Bwana aliwaamuru Waisraeli zamani wasioane na watu wa mataifa yenye kuabudu miungu ya kishenzi waliokuwa wamewazunguka: “Wala usioane nao, binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake.” Sababu yake imetolewa. Mungu, akiwa mwenye kuona mbele matokeo ya baadaye ya umoja wa namna hii, asema: “Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi.” “Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako; Bwana Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.” KN 139.3
Katika Agano Jipya kuna maneno yanayokataza Wakristo kuoana na makafiri. Mtume Paulo, katika waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho, asema: “Mwanamke hufungwa maadamu mumewe yu hai, lakini ikiwa mumewe amefariki, yu huru kuolewa na mtu ye yote amtakaye; katika Bwana tu. ” Tena, katika waraka wake wa pili, ameandika: “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi lsivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliali? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana si tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, tokeni kati yao, mkatengwe nao, asema Bwana, msiguse kitu kilicho kichafu, nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike asema Bwana Mwenyezi.” KN 139.4
Kamwe watu wa Mungu wasingethubutu kuingia mahali Palipokatazwa na Mungu. Ndoa baina ya waaminio na wasioamini imekatazwa na Mungu. Lakini mara nyingi moyo usioongoka hufuata tamaa zake wenyewe, na ndoa zisizokubaliwa na Mungu hufanywa. Kwa sababu hii wanaume na wanawake wengi hawana tumaini wala hawanaye Mungu ulimwenguni. Mivuto yao bora imekufa; kwa mnyororo wa hali ya mambo haya wameshikwa wavuni mwa Shetani. Wale wanaotawaliwa na ashiki na taama mbaya ya mwili watakuwa na mavuno machungu kuvuna katika maisna haya, na mwenendo wao waweza kuleta hasara ya roho zao mwishowe. KN 140.1
Wale wanaoungama kweli huyakanyaga mapenzi ya Mungu kwa kuoana na wasiaoamini; wanapoteza kibali cha Mungu na kufanya kazi ngumu kwa kutubu. Huenda mtu asiyeamini akawa mwenye tabia njema ya moyoni, lakini kwamba hajaungama majibu ya madai ya Mungu naye amekataa wokovu mkuu namna hii ni sababu ya kutosha inayoacha umoja usikamilishwe. Pengine tabia ya yule asiyeamini huenda ikafanana na ile ya yule kijana ambaye Yesu alimwambia maneno haya, “Umepungukiwa na neno moja;” hilo lilikuwa neno moja lenye kutakikana sana. KN 140.2