Vita Kuu
Sura Ya Kumi Na Tisa - Ujira Wa Watakatifu
*****
HALAFU niliona jeshi la malaika wengi sana wakizileta taji za utukufu kutoka katika mji mtakatifu —taji moja kwa kila mtakatifu, na jina lake limeandikwa juu yake. Yesu alipoziagiza taji, malaika walizileta kwake, naye kwa mkono wake wa kulia aliziweka vichwani mwa watakatifu. Vile vile malaika walivileta vinanda na Yesu alivigawa kwa kila mtakatifu. Malaika wenye cheocha juu waliongoza kwa kupiga vinanda, ndipo sauti zote zikainuliwa kwa sifa na shukrani, na kila mkono ukaanza kuzinyakua nyuzi za vinanda, kama wajuzi kamili wa muziki, vikatoa sauti tamu na za kupendeza. VK 121.1
Ndipo nikamwona Yesu akiwaongoza wale waliookolewa kwenye mlango wa mji. Aliushika mlango akaujongeza nyuma kwa pata zake zilizokuwa ziking’aa, akawaambia mataifa yote yaliyozishika amri zake waingie ndani. Kila kitu kilichokuwa mjini kilikuwa cha kupendeza macho. Utukufu mwingi ulionekana kila mahali. Ndipo Yesu akawaangalia watakatifu wake Waliookolewa; nyuso zao ziling’aa kwa utukufu; naye alipokaza macho ya upendo juu yao akasema kwa sauti yake iliyo tamu: “Nayaona masumbufu ya moyo wangu. na nimeridhika. Utukufu huu wa ajabu ni wenu, nanyi mtaufurahia milele. Huzuni zenu zimekoma. Haitakuwako mauti tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena” Naliwaona waliokolewa wakiinama wakizitupa taji zao miguuni pa Yesu, na alipowainua kwa mkono wake wa upendo, wakavichukua vinanda vyao vya dhahabu wakazijaza mbingu na sauti tamu ya muziki wakimwimbia MwanaKondoo. VK 121.2
Baadaye nikamwona Yesu akiwaongoza watu wake kwenye mti wa uzima, na tukasikia tena sauti yake ya kupendeza, sauti nzuri zaidi ya sauti yo yote ambayo wanadamu wamepata kuisikia, akiscma, “Majani ya mti huu yatakuwa kwa kuwaponya mataifa. Mnaruhusiwa kuyala yote.” Mti wa uzima ulizaa matunda mazuri ajabu, ambayo watakatifu waliruhusiwa wayale kwa wingi, katika mji kulikuwa na kiti cha enzi cha Mungu, ulipotoka mto wa maji ya uzima, yaliyokuwa safi kama kioo. Kila upande wa mto huu kulikuwa na mti wa uzima, na katika kingo za mto huu kulikuwa na miti mingine mizuri iliyokuwa na matunda ambayo pia yalikuwa matamu kwa chakula. VK 122.1
Lugha za kibinadamu hazitoshi hata kujaribu kusimulia jinsi mbingu ilivyo. Kama nikiwaza mambo haya jinsi nilivyoonyeshwa, nashangaa kabisa. Nikivutwa moyoni kwa ajili ya utukufu ule na fahari ya ajabu, naiweka kalamu chini, nikisema, “Lo, si upendo huu! wa ajabu kabisa!” Lugha iliyo bora zaidi duniani haiwezi kuusimulia utukufu wa mbinguni na upendo usiokadirika wa Mwokozi wetu. VK 122.2