Vita Kuu

45/56

Marejeo ya Yesu

Mara likaonekana wingu kuu lililo jeupe, na juu yake aliketi Mwana wa Adamu. Wingu hili lilipoonekana kwa mbali, lilikuwa dogo sana. Malaika alisema ya kwamba lilikuwa ishara ya Mwana wa Adamu. Liliposhuka na kuzidi kukaribia dunia, tuliweza kuuona uzuri na utukufu kamili wa Yesu alipoondoka apate kushinda. Jeshi la malaika watakatifu wenye taji zing’aazo vichwani, wakafuatana naye. VK 118.3

Hakuna lugha yo yote inayoweza kusimulia fahari na utukufu wa mambo hayo jinsi yalivyo. Wingu lile la utukufu wa ajabu, ambalo lilikuwa jeshi la malaika watukufu, liliendelea kuikaribia dunia hata tuliweza kumwona Yesu mwenyewe dhahiri na uzuri wake. Hakuvaa taji ya miiba, bali taji ya utukufu ilikuwa kichwani mwake. Katika vazi lake na katika paja lake liliandikwa jina, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana. Uso wake uling’aa kama mwangaza wa jua wakati wa adhuhuri, macho yake yalikuwa kama mwako wa moto, na miguu yake ilionekana kama shaba iliyo safi sana. Sauti yake ilisikika kama sauti za vinanda vingi. Dunia ilitetemeka mbele yake, mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake. “Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na mwungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima, wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwana-Kondoo. Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani avvezaye kusimama?” Ufunuo 6:15-17. VK 119.1

Wale ambao muda kitambo kabla ya wakati ule walikuwa tayari kuwaharibu waaminifu wa Mungu duniani, sasa waiiona wenyewe utukufu wa Mungu uliowakalia. Hao nao walipokuwa wanashikwa na hofu nyingi sana, walisikia sauti za watakatifu wakisema kwa furaha, “Huyu ndiye Mungu wetu, ndiye tuliyemngojea, atusaidie.” Isaya 25:9. VK 119.2