Vita Kuu

32/56

Ujumbe wa Kutisha

Onyo la kutisha zaidi na la kuogofya ambalo limetolewa kwa wanadamu ni lile lililoandikwa katika ujumbe wa malaika wa tatu. Dhambi ambayo inaleta ghadhabu ya Mungu isiyochanganyika na rehema, bila shaka ni dhambi mbaya sana. Wanadamu hawawezi kuachwa gizani bila kuonywa juu ya jambo hili kuu; onyo juu ya dhambi hii halina budi kutolewa kwa walimwengu kabla ya wakati wa hukumu za Mungu, kusudi wote wajue kwa nini hukumu zinatolewa, na wapate kuwa na nafasi ya kuepukana na adhabu hizo. VK 86.1

Katika mwisho wa shindano hili kuu, inabainika aina mbili za watu walio mbali mbali kabisa. Aina ya kwanza ndio wanaomsujudu “huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea alama katika kipaji cha uso,” na hivi kujiletea hukumu mbaya iliyotangazwa na malaika wa tatu. Aina ya pili ndio “wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” Ufunuo 14:9, 12. VK 86.2

Haya ndiyo mafundisho makuu yaliyofunuliwa kwa wale walioupokea ujumbe wa malaika wa tatu. Walipotazama nyuma na kufikiri mambo yaliyotendeka kwao tangu walipoanza kutangaza habari za kuja kwa Kristo mara ya pili mpaka kupita kwa wakati ule katika mwaka wa 1844, waliona ya kwamba uchungu wao ulikuwa umeelezwa na mioyo yao ilianza tena kujaa tumaini na furaha. Nuru iliyotoka katika patakatifu iliyaangaza mambo yaliyopita, mambo yaliyopo, na mambo yajayo, hao nao wakafahamu ya kwamba Mungu alikuwa amewaongoza kwa njia yake iliyo ya haki. Sasa kwa ushujaa na imani thabiti, waliungana kwa kuyatoa maonyo ya malaika wa tatu. Tangu mwaka wa 1844, kwa kuutimiza unabii wa ujumbe wa malaika wa tatu, watu wa dunia wameelekezwa habari ya Sabato ya kweli, na watu wengi huongezeka daima wa kimdi wapate kuitunza siku ya Mungu iliyo takatifu. VK 86.3