Tumaini la Vizazi Vyote

57/307

Maombi ya siri ya Nathanael yalisikiwa

Filipo alipomwita, Nathanael alikuwa ametoka kuomba katika kichaka, na kutafakari juu ya unabii, unaohusu kuja kwa Masihi . . . aliomba kwamba, kama huyo anayehubiriwa na Yohana Mbatizaji ndiye Mkombozi, basi afahamishwe. Roho Mtakatifu akamjilia, akamhakikishia kuwa, Mungu alikuwa amewajilia watu wake. Filipo alifahamu kuwa rafiki yake alikuwa akichunguza unabii, na wakati Nathanaeli alipokuwa akiomba kichakani, Filipo alimwona. Kila mara walikuwa wakiomba pamoja kwa siri mahali pa maficho, TVV 71.1

Ujumbe kwamba, “Tumemwona Masihi,” ambaye alinenwa na Musa na kuandikwa katika sheria yake, na manabii, kwa Nathanaeli ilionekana kwamba, ndilo jawabu wazi la sala yake. Lakini Filipo alipoongeza na kusema, “Yesu wa Nazareti, mwana wa Yusufu,’ Nathanael alichukizwa, na kusema, “je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?” TVV 71.2

Filipo akasema, ‘Njoo, uone.” Yesu alimwona Nathanael akimjia, akasema, “Tazama, huyu ndiye Mwisraeli halisi asiye na ila! Nathanael akasema kwa mshangao, “Ulinifahamu lini?” Yesu akajibu, “Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwa chini ya mti, nilikuona.” TVV 71.3

Ilitosha Roho wa Mungu aliyeshuhudia kwa Nathanael alipokuwa akiomba mahali pa siri chini ya mti, alimzungumzia katika maneno ya Yesu. Nathanaeli alikuja kwa Yesu akiwa na shauku ya ukweli, na sasa ametosheka, na shauku yake imekwisha. Alisema, “Rabi, wewe ni Mwana wa Mungu; Wewe u Mfalme wa Israeli!” TVV 71.4

Kama Nathanaeli angaliwategemea walimu wa Kiyahudi ili wamwongoze, asingalimwona Yesu kamwe. Alikuwa mfuasi kwa ajili ya kuona na kuamua yeye mwenyewe. Na leo ni vivyo hivyo. Watu wengi huwategemea wanadamu walio waongozi. Inatupasa tusome neno la Mungu sisi wenyewe kama Nathanaeli alivyofanya, na kuomba ili tupate uvuvio wa Roho Mtakatifu. Aliyemwona Nathanaeli akiomba chini ya mti hutuona sisi pia tunapokuwa tukiomba mahali pa siri. Malaika huwa karibu na wale wanaomtafuta Mungu kwa unyenyekevu, ili awaongoze. TVV 71.5

Katika kuitwa kwa Yohana, Andrea, Simoni, Filipo na Nathanaeli, ndipo ulianzishwa msingi wa kanisa la Kristo. Yohuna Mbatizaji aliwapeleka wanafunzi wake wawili kwa Kristo. Halafu mmojawapo wa wanafunzi hao, yaani Andrea, alimpata ndugu yake. Kisha Filipo aliitwa, naye akaenda kumtafuta Nathanaeli. Mfano huu unatufundisha fundisho muhimu sana, kuhusu jinsi ya kuwaita jamaa zetu, marafiki zetu, na majirani zetu. Wako watu ambao hawajajaribu kamwe kufanya bidii kuleta hata mtu mmoja kwa Kristo. TVV 71.6

Wengi wamepotea bila tumaini, ambao wangaliokolewa kama majirani zao, watu wa kawaida tu wangalijitahidi kuwashughulikia. Katika jamaa, ujirani, na katika miji tunapoishi, kuna kazi inayotupasa kufanya. Mara mtu unayemshughulikia akiongoka, naye hutamani kuwashughulikia wengine. Akimpata mtu huwa rafiki yake wa thamani katika Kristo. TVV 72.1