Tumaini la Vizazi Vyote

165/307

Kristo ndiye Mwamba

Musa alikuwa ameonyesha mwamba wa wokovu wa Israeli. Tazama Torati 32:4. Zaburi imeimba juu ya “Mwamba wa nguvu zangu.” Zaburi 62:7. Isaya alikuwa ameandika: “. . . Tazama naweka katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, . . . Isaya 28:16. Petro mwenyewe aliutaja unabii huu kumhusu Yesu. Maana ninyi mmeonja wema wa Bwana. Njooni kwake, ambaye ndiye jiwe lililo hai, lililokataliwa na watu, lakini kwa Mungu ni jiwe teule, lenye thamani. Na ninyi kama mawe yaliyo hai, mmejengwa katika hekalu la kiroho. Soma 1 Petro 2:3-5. TVV 233.2

“Maana msingi mwingine hakuna awezaye kuuweka isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani Yesu Kristo.” 1 Wakorintho 3:11. Yesu alisema, “Juu ya mwamba huu, nitalijenga kanisa langu.” Kristo alijenga kanisa lake juu ya mwamba yaani juu yake mwenyewe, mwili watte, umevunjwa kwa ajili yetu. Juu ya kanisa lililojengwa juu ya msingi wake mwenyewe, milango ya kuzimu haitalishinda. TVV 233.3

Wakati Kristo aliposema maneno haya kanisa lilionekana kuwa dhaifu kiasi gani ulimwenguni! Kulikuwa na wafuasi wachache sana, ambao watakabiliana na nguvu za Shetani na wanadamu pia. Walakini hawataogopa, hakuna kitu kitakachowashinda. TVV 233.4

Petro alikuwa amesema ukweli ambao ni msingi wa kanisa na imani yake, na Yesu alimsifu kama mjumbe wa kweli badala ya kundi la waamini wote. “Nami nitakupa funguo za ufalme wa mbinguni: Lolote utakaolifunga duniani Utakuwa limefungwa mbinguni, na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.” TVV 233.5

“Funguo za ufalme wa mbinguni, ni maneno ya Kristo. Maneno yote ya Biblia ni yake. Maneno haya yana nguvu za kufungua na kufunga mbingu. Kazi ya wale wanaohubiri neno la Mungu huleta uzima au mauti. TVV 233.6

Mwokozi hakumkabidhi kazi Petro, kama mtu binafsi, yaani kazi ya kuhubiri Injili. Baadaye aliporudia kusema maneno hayo tena yaliyosemwa kwa Petro, Mwokozi aliyasema kwa kanisa zima, na kwa mitume kumi na wawili ambao walikuwa wawakilishi wa kundi zima la kanisa. Kama Yesu angalimkabidhi mtu mmoja ujumbe maalum zaidi ya wengine wote, tusingeona wakibishania ukubwa. Wangalimheshimu mtu aliyekabidhiwa tu. Badala ya kumteua mtu mmoja kuwa mkuu wao, Kristo alisema: “Msiitwe Rabi, . . . wala msiitwe mabwana, maana Bwana wenu ni mmoja tu, ndiye Kristo.” Mathayo 23:8, 10. TVV 233.7

Kichwa cha kila mtu ni Kristo. Mungu aliweka vitu vyote chini ya miguu ya Mwokozi, akamweka awe kichwa cha mambo yote kanisani, ambalo ni mwili wake, ambaye ni utimilifu wake katika mambo yote. Soma 1 Wakorintho 11:3; Waefeso 1:22, 23. Kanisa limejengwa kwa Kristo, aliye msingi wake. Kanisa haliwezi kumtegemea mtu, au haliwezi kutawaliwa na mtu. Watu wengi hudhani kuwa cheo walicho nacho kanisani, huwafanya wawe wenye uwezo wa kuwaamuru washiriki jinsi ya kufanya. Mwokozi alisema, Ninyi nyote ni ndugu, tazama Mathayo 23:8. Hakuna mtu yeyote au kiumbe chochote tunachoweza kutegemea ili kituongoze. Mwamba wa imani ni kuwako kwa Kristo kanisani. Wanaojidhania kuwa wana nguvu, wataonekana kuwa ni wanyonge mno, wasipomweka Kristo kuwa nguvu zao. Soma Yeremia 17:5; Zaburi 2:12. TVV 234.1

Yesu aliwagiza wanafunzi wake kwamba wasimwambie mtu yeyote kuwa wao ndio Kristo. Watu walikuwa na mawazo ya makosa kumhusu Masihi. Hata wanafunzi wake pia hawakuwa na ufahamu wa wazi. Mawazo ya watu na usemi wao ungewakosesha wasitambue tabia yake, na kazi yake. TVV 234.2