Mashujaa wa Imani

1/21

Mashujaa wa Imani

1—Sulemani

WAKATI wa utawala wa Daudi na Sulemani, Waisraeli walikuwa watu wakuu, hodari kati ya mataifa, nao walikuwa na nafasi nyingi za kueneza mvuto mkubwa wa kuelekea katika kweli na haki. Jina la Yehova lilitukuka na kuheshimiwa, na makusudi ya kuwakalisha Waisraeli katika nchi hiyo ya ahadi yalikuwa yanatimizwa. Mapingamizi yaliondolewa, na watu waliokuja kutoka katika nchi za mataifa ili kutafuta kweli walipata walichotaka bila wasiwasi. Watu walitubu, na kanisa la Mungu duniani lilizidi na kustawi. MwI 7.1

Wakati wa mwisho wa utawala wa Daudi, Sulemani alitiwa mafuta awe mfalme, mahali pa baba yake aliyejiuzulu. Mwanzoni mwa maisha yake mambo yalikuwa bora sana, na lilikuwa kusudi la Mungu kwamba azidi na kuendelea, huku akielekea kwenye tabia ya Mungu, hivyo apate kuwatia moyo watu wake watimize kazi yao takatifu kama watunzaji wa kweli za Mungu. MwI 7.2

Daudi alijua kwamba makusudi makuu ya Mungu kwa Waisraeli yangetimia tu wakati Watawala na raia watakapojitahidi bila kukoma kufikia kiwango walichowekewa. Alijua kuwa, ili kusudi mwanawe Sulemani aweze kufikia na kutimiza mambo matakatifu ya Mungu, haikumpasa kijana awe mtu wa kupigana vita, na kuamua mashauri tu na kutawala, bali ilimpasa awe mtu hodari, mwema, mwalimu afundishaye haki, ili awe kielelezo cha kuigwa na wengine. MwI 7.3

Basi Daudi alimsihi mwanawe kwa upole na unyenyekevu, awe mtu mwema, mwungwana, akionyesha moyo wa rehema na fadhili kwa raia zake, na kwa mataifa yote ya dunia awe kielelezo halisi, ili waliheshimu na kulitukuza jina la Mungu katika uzuri wa utakatifu. Mambo mengi magumu ambayo Daudi alikutana nayo katika maisha yake, yalimfundisha kuwa mwenye huruma na fadhili, nayo yalimwezesha kusema kwa uthabiti maneno hayo ya mausia siku zake za mwisho: “Atawalaye wanadamu kwa haki, akitawala katika kicho cha Mungu, atakuwa kama nuru ya asubuhi jua lichapo, asubuhi isiyo na mawingu. Lachipuza majani mabichi juu ya nchi, kwa mwangaza baada ya mvua.” 2 Samweli 23:3, 4. MwI 8.1

Lo, ilikuwa bahati gani kwa Sulemani! Kama angefuata mausia ya baba yake, ambayo ni mausia ya Mungu, utawala wake ungekuwa utawala wa haki, kama vile unavyoelezwa katika Zaburi 72: MwI 8.2

“Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu.
Milima itawazalia watu amani,
Na vilima navyo kwa haki.
Atawahukumu walioonewa wa watu,
Atawaokoa wahitaji, atamseta mwenye kuonea.
Watakuogopa wakati wote wa kudumu jua,
Na wakati wa kung'aa mwezi kizazi hata kizazi.
Atashuka kama mvua juu ya majani yaliyokatwa,
Kama manyunyu yainyweshayo nchi
Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka mto hata miisho ya dunia. Wakaao jangwani na wainame mbele zake;
Adui zake na warambe mavumbi.
Wafalme wa Tarshishi na visiwa na walete kodi;
Watalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa.
Naam, wafalme wote na wamsujudie;
Na mataifa yote wamtumikie.
Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
Na nafsi za wahitaji ataziokoa.
Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu,
Na damu yao ina thamani machoni pake.
Basi na aishi
Na wampe dhahabu ya Sheba;
Na wamwombee daima;
Na kumbariki mchana kutwa.
Na uwepo wingi wa nafaka
Katika ardhi juu ya milima;
Matunda yake na yawaye —waye kama Lebanoni,
Na watu wa mjini wasitawi kama majani ya nchi.
Jina lake na lidumu milele,
Pindi ling'aapo jua jina lake liwe na wazao;
Mataifa yote na wajibariki katika yeye,
Na kumwita heri.
Na ahimidiwe Bwana, Mungu, Mungu wa Israeli,
Atendaye miujiza Yeye peke yake;
Jina lake tukufu na lihimidiwe milele;
Dunia yote na ijae utukufu wake. Amina na Amina.”
MwI 8.3

Wakati wa ujana wake, Sulemani alichagua kufuata njia zile zile za Daudi, na kwa muda wa miaka mingi alienenda kikamilifu, akiyatii maagizo ya Mungu kabisa. Mwanzoni mwa utawala wake, alikwenda Gibeoni pamoja na washauri wake, mahali ambapo hema ya maskani iliyofanywa huko jangwani ilikuwa ikikaa, yeye pamoja na “Israeli wote, na maakida wa maelfu, na wa mamia, na waamuzi na kila shehe wa Israeli wote, wakuu wa nyumba za mababa,” wakamtolea Mungu dhabihu, na kujiweka wakfu ili wamtumikie Bwana. 2 Mambo ya Nyakati 1:2. Sulemani akifahamu uzito na umuhimu wa kazi ya utawala na matatizo yake, aliona sababu ya lazima inayowalazimisha wote wanaobeba mizigo ya jinsi hiyo kutafuta hekima na uongozi wa mbinguni ikiwa wanataka kufaulu katika madaraka hayo. Jambo hili lilimfanya awatake washauri wake, ili wajiunge pamoja katika kuutafuta ukubali wa Mungu. MwI 9.1

Mfalme alitafuta hekima ya mbinguni na ufahamu, ili aweze kutenda kazi yake kwa ukamilifu, kuliko kutafuta utajiri na heshima. Alitamani kuwa na akili yenye kutambua mambo kwa upesi, na uthabiti wa kuwa na utu wema. Usiku huo, Bwana alimtokea katika ndoto, akasema, “Omba utakalo, nikupe.” Katika kuiibu, mfalme kijana, asiyejua mengi, alitaja namna asivyokuwa na uwezo wa kutimiza wajibu wake katika kazi kubwa Bwana aliyompa, kwamba anahitaji msaada. Akasema, “Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niw ahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuw ahukumu hawa watu wako walio wengi? MwI 10.1

“Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili.” MwI 10.2

“Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako wala hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha ya wakuchukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwahukumu watu wangu, niliokutawaza juu yao; basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.'. MwI 10.3

“Nawe ukienda katika njia zangu, na kuyashika mausia yangu, na amri zangu. kama baba yako Daudi alivyokwenda, basi nitazifanya siku zako kuwa nyingi.” 1 Wafalme 3:5-14; 2 Mambo ya Nyakati 1:7-12. MwI 11.1

Mungu aliahidi kwamba, kama vile alivyokuwa pamoja na Daudi vivyo hivyo atakuwa pamoja na Sulemani. Kama mfalme Sulemani akienenda kwa unyofu mbele za Mungu na kutenda yote anayoamriwa na Bwana, kiti chake kingeimarishwa, na utawala wake ungekuwa njia ya kuwatukuza Waisraeli kuwa hekima na akili machoni pa mataifa.” Kumbukumbu la Torati 4:6. MwI 11.2

Lugha Sulemani aliyotumia wakati alipokuwa akiomba madhabahuni huko Cibeoni, inadhihirisha jinsi alivyokuwa na nia ya kumtafuta na kumtumikia Mungu. Alifahamu kuwa pasipo msaada wa Mungu, asingefaulu kutimiza kazi ile Mungu aliyomtwika, maana alikuwa sawa sawa na mtoto ambaye hawezi lo lote. Alijua kuwa alipungukiwa na akili ya utambuzi, hivyo ilikuwa nia yake kutafuta hekima itokayo juu. Hakuwa na nia yo yote ya kutafuta makuu, wala kujitukuza, maana hakuwa na hali ya kujifikiria yeye binafsi. MwI 11.3

Alichotaka ni hekima ya kufanya kazi yake kwa uaminifu na haki. Naye alichagua njia itakayolitukuza jina la Mungu, kwa ajili ya utawala wake. Sulemani hajakuwa kamwe mwenye utajiri au hekima an sifa zaidi kama wakati ule alipokiri ya kwa alikuwa “mtoto mdogo tu, asiyejua jinsi ampasavyo kutoka wala kuingia.” MwI 11.4

Watu ambao wanashikilia madaraka siku hizi hawana budi kupata fundisho kutokana na sala ya Sulemani. Kadiri mtu anavyopanda cheo, ndivyo madaraka yake yanavyozidi, na mvuto wake hupanuka zaidi, na yeye humhitaji Mungu zaidi amwongoze. Daima hukumbuka kwamba, anapoitwa kuchukua madaraka makuu, papo hapo huwa na wajibu wa kuwatendea wenzake kwa uangalifu mwingi na hadhari. Hana budi kusimama mbele za Mungu akiwa katika hali ya mwanafunzi anayehitaji kufundishwa. Kuwa na cheo kikubwa hakuongezi ubora wa tabia. Mtu hupata ukuu wa kweli kwa njia ya kumheshimu Mungu na kuyatii maagizo yake. MwI 11.5

Mungu tumtumikiaye hana upendeleo kwa mtu ye yote. Mungu yule aliyempa Sulemani hekima, yuko tayari kuwapa watoto wake hekima na ufahamu siku hizi. Neno lake husema, “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.” Yakobo 1:5. Mtu achukuaye madaraka akitamani hekima kuliko kutamani utajiri na ukuu au cheo hatanyimwa. Mtu kama huyo atajifunza kutoka kwa Mwalimu Mkuu, si mambo ya kutenda tu, ila na jinsi ya kuyatenda pia ili, yakubaliwe na Mungu. Muda mtu aliyepewa busara na uwezo anakuwa amejitoa kwa Mungu, hataonyesha nia yo yote ya kutaka cheo kikuu, wala kujitukuza juu ya wengine kama mtawala mkuu. Watu lazima wachukue madaraka; lakini badala ya kutaka makuu na heshima, kiongozi wa kweli hana budi kuomba, ili apewe moyo wa kufahamu na kupambanua kati ya mema na mabaya. MwI 12.1

Njia ya watu wenye kusimamia si nyepesi. Lakini wenye madaraka lazima wakimbilie maombi wakati wote mambo yanapowawia magumu. Wasikae mbali na chemchemi ya hekima zote. Mkuu wa wakuu wote, akiwatia nguvu na kuwaangazia, watawezeshwa kusimama imara na kuipinga mivuto ya mwovu, na watatambulisha na kupambanua kati ya haki na makosa, na kati ya mema na mabaya. Watafuata mambo yale yanayompendeza Mungu tu, nao watajitahidi kupinga kila kosa linaloelekea kuingia katika mambo ya Mungu. MwI 12.2

Sulemani alipewa na Mungu hekima aliyotamani zaidi ya mali, heshima, au maisha marefu. Alipewa akili ya utambuzi, ushujaa, na utu wema, yaani roho yenye huruma. “Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu, kama mchanga ulioko pwani. Hekima ya Sulemani hekima, ikapita hekima ya wana wote wa mashariki, na hekima zote za Misri. Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote. . . . Zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka.” 1 Wafalme 4:29-31. MwI 12.3

“Na Israeli wote . . wakamwogopa mfalme, maana waliona ya kuwa hekima ya Mungu ilikuwa ndani yake, ili afanye hukumu.” 1 Wafalme 3:28. Mioyo ya watu ikamgeukia Sulemani, kama walivyokuwa kwa Daudi, nao wakamtii katika mambo yote. “Basi Sulemani . . . alithibitishwa katika ufalme wake, naye Bwana, Mungu wake, alikuwa pamoja naye, akamtukuza mno.” 2 Mambo ya Nyakati 1:1. MwI 12.4

Kwa muda wa miaka mingi maisha ya Sulemani yalikuwa ya kumtii Mungu, akifuata kanuni za haki na kuzitii amri zake. Katika mambo yote yahusianayo na kazi yake ya utawala aliyaongoza vema sana. Utajiri wake, hekima yake, na majengo mashuhuri aliyoyajenga, na kazi nyingine alizofanya mwanzoni mwa utawala wake, bidii yake, na unyofu wake pamoja na haki na utu wema wake ambavyo vilidhihirika wazi kwa maneno na matendo yake, viliwavuta raia zake wamwamini kabisa; hata na wafalme wa nchi nyingine walimheshimu sana. MwI 13.1

Wakati wa sehemu ya kwanza ya utawala wa Sulemani jina la Mungu liliheshimiwa na kutukuzwa sana. Hekima ya mfalme na matendo yake ya haki aliyoyatenda yalishuhudia juu ya ukuu wa Mungu kwa mataifa yote, kwamba Mungu wa Sulemani ndiye Mungu wa kweli. Kwa muda wa miaka kadhaa Waisraeli walikuwa nuru ya ulimwengu wakiuonyesha utukufu wa Mungu na ukuu wake. Siyo hekima yake, wala utajiri wake, wa nguvu zake, wala heshima yake kwamba ndivyo vilivyomletea sifa na utukufu, bali ni kwa ajili ya kulitukuza jina la Mungu wa Israeli kwa njia ya kutumia kwa hekima vipawa alivyopewa na Mungu. MwI 13.2

Kadiri miaka ilivyopita ndivyo Sulemani alivyozidi kuongeza kumtukuza Mungu zaidi na zaidi, naye akiongeza nguvu zake za kiroho na kimawazo alishirikisha mibaraka hiyo kwa wengine. Hakuna mtu aliyefahamu zaidi yake kwamba, amefikia hali hiyo kwa ajili ya rehema na upendo wa Yehova, na kwamba amepata mibaraka hiyo, ili aujulishe ulimwengu kuhusu Mfalme wa Wafalme MwI 13.3

Sulemani alipenda sana kuchungua mambo ya asili; lakini uchunguzi wake haukuhusu sehemu fulani tu, bali zote. Kwa kuvichunguza viumbe hai na visivyo hai, alipata ufahamu halisi juu ya uumbaji na Mwumbaji. Kwa kuangalia sheria za asili zinazotawala ulimwengu habari za madini, na wanyama, kwa kuangalia miti na maua na vichaka, aligundua hekima ya Mungu. Na kwa jinsi alivyoendelea kujifunza zaidi na zaidi juu ya viumbe, utambuzi wake juu ya Mungu uliongezeka na upendo wake kwa Mungu ulizidi daima. MwI 13.4

Hali ya kiroho ya Sulemani inaonekana katika nyimbo za kusifu na mithali alizotunga. “Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano. Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.” 1 Wafalme 4:32, 33. MwI 14.1

Katika mithali za Sulemani zimo kanuni za maisha matakatifu na makusudi makuu, zimo kanuni ambazo ni za mbinguni, zinazoongoza mtu mpaka kwenye utawa; kanuni zifaazo ziongoze matendo yote ya mtu na maisha yake. Ni kwa ajili ya kueneza kanuni hizo na kumtambua Mungu kuwa ndiye anayestahili heshima na sifa, ndiko kulimfanya Sulemani akafanikiwa wakati wa mwanzo wa utawala wake. Alifanikiwa kiroho na kiuchumi. MwI 14.2

Aliandika, “Heri mtu yule aonaye hekima, na mtu yule apataye ufahamu. Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi. Yeye ana thamani kuliko marijani, wala vyote avitamanivyo havilingani naye. Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto. Njia zake ni njia za kupendeza sana, na mapito yake yote ni amani. Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana, ana heri kila mtu ashikamanaye naye.” Mithali 3:13-18. MwI 14.3

“Bora hekima, basi jipatie hekima; naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu.” Mithali 4:7. “Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima.” Zaburi 111:10. “Kumcha Bwana ni kuchukia uovu; kiburi na majivuno, na njia mbovu, na kinywa cha ukaidi pia nakichukia.” Mithali 8:13. MwI 14.4

Lo, kama Sulemani angeyashika mausia hayo katika siku zake za mwisho za utawala wake, ingekuwa heri! Ndiye aliyesema, “Ndiye aliyesema, “Midomo ya mwenye haki hueneza maarifa.” (Mithali 15:7). Yeye aliyewafundisha wafalme wa dunia kumtolea heshima na sifa Mfalme wa mbinguni ambaye ni Mfalme wa wafalme, ingekuwa bora kama asingalijivuna, na mwenye kinywa cha ukaidi kujitwalia heshima na sifa, ambavyo vinamstahili Mungu peke yake! MwI 14.5