Tumaini Kuu

85/254

Moyo wa Wesley Wapata Joto kwa Njia ya Ajabu

Aliporudi Uingereza, Wesley alifikia mahali pa kuielewa imani ya Biblia kwa ufasaha zaidi chini ya usimamizi wa Wamoravia. Kwenye mkutano wa jumuia ya Wamoravia mjini London tamko la Luther lilisomwa. Alipokuwa anasikiliza, imani iliamshwa ndani ya moyo wa Wesley. Anasema “Nilijisikia moyo wangu ukipata joto kwa njia ya ajabu, nilijisikia kumtumainia Yesu, Yesu peke yake, kwa wokovu na nilipewa uthibitisho, kwamba ameziondoa dhambi zangu, hata mimi mwenyewe, na ameniokoa toka kwenye sheria ya dhambi na mauti.” 164 TK 166.1

Na sasa alitambua kuwa ile neema aliyokuwa anaitaabikia kuipata kwa maombi, na kwa kufiinga, na kwa kujitesa ilikuwa inatolewa bure, “bila pesa na bila kima chochote.” Moyo wake ulijaa hamasa na shauku ya kuisambaza kila mahali Injili tukufu ya Mungu na neema yake inayopatikana bure. “Ninauangalia ulimwengu wote kama parokia yangu,” alisema; “katika sehemu yoyote nitakayokuwa, naona kuwa ni vema, ni haki, na ni wajibu wangu, kuwatangazia wale wote walio tayari kusikia habari njema za wokovu.” 165 TK 166.2

Aliendelea na maisha yake ya utii na kujikana nafsi, kwa wakati huu yakiwa si msingi, lakini kama matokeo ya imani, si mzizi, lakini tunda la maisha matakatifu. Neema ya Mungu katika Kristo itadhihirishwa kwa utii. Wesley alikuwa ameyatoa maisha yake kuhubiri ukweli mkuu aliokuwa ameupokea-kuhesabiwa haki kwa njia ya imani kwa upatanisho wa damu ya Kristo, na moyo kufanywa upya kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, na kuzaa matunda maishani yanayopatana na kielelezo cha maisha ya Kristo. TK 166.3

Whitefield na wafuasi wa Wesley walikuwa wanaitwa kwa kebehi “Wamethodisti” na wanafunzi wenzao wasiokuwa wacha Mungu-jina linalochukuliwa kuwa ni la heshima kubwa katika siku zetu. Roho Mtakatifu alikuwa anawahimiza kumhubiri Kristo, Yeye aliYesulubishwa. Maelfu waliongolewa. Lilikuwa ni jambo la lazima kuwapatia kondoo hawa wa Mungu ulinzi dhidi ya mbwa mwitu wakali. Wesley hakuwa na wazo la kuanzisha dhehebu jingine jipya, lakini aliwaweka pamoja watu hawa kwa kile kilichokuwa kinaitwa Muunganiko wa Wamethodisti. TK 167.1

Upinzani waliokuwa wanaupata wahubiri hawa kutoka kwenye kanisa lililokuwepo ulikuwa wa kisirisiri na wenye majaribu mengi-lakini bado ukweli uliweza kuingia katika milango ambayo vinginevyo ingebaki imefungwa. Baadhi ya wachungaji waliamka toka kwenye usingizi wao wa kimaadili na kuwa wahubiri hodari katika parokia zao. TK 167.2

Zama za Wesley watu waliokuwa na karama mbalimbali hawakuyafanya mafundisho yao kuwa na ulinganifu. Tofauti zilizokuwepo kati ya Whitefield na wafuasi wa Wesley vilitishia kuleta mfakarano mkubwa, lakini kwa kadri walivyojifunza unyenyekevu katika shule ya Kristo, kustahimiliana na kupendana kuliieta mapatano kwa pande hizi mbili. Hawakuwa na muda wa mafarakano wakati kila mahali makosa na uovu vilikuwa vinaendelea kutapakaa. TK 167.3