Tumaini Kuu

79/254

Sura Ya 14 - Maendeleo Ya Ukweli Uingereza

W akati Luther anaifungua Biblia iliyokuwa imefungwa kwa watu wa Ujerumani, Tyndale alikuwa anahimizwa na Roho wa Mungu kufanya yayo hayo nchini Uingereza. Biblia ya Wycliffe ilikuwa imetafsiriwa kutoka kwenye Maandiko ya Kilatini, yaliyokuwa na makosa mengi. Gharama za nakala za miswada ilikuwa kubwa mno kiasi cha kufanya usambazaji wake kuwa mdogo. TK 159.1

Mnamo mwaka 1516, Agano Jipya lilichapishwa kwa mara ya kwanza katika lugha yake ya asili, yaani Kigiriki. Makosa mengi ya nakala zilizokuwa zimepita yalisahihishwa, na Maandiko yalikuwa yanaeleweka vizuri na kwa uwazi zaidi. Hili liliwaongoza wengi wa wanazuoni kuelewa vizuri elimu ya ukweli na kutoa msukumo mpya kwa kazi ya matengenezo. Kwa kiasi kikubwa, watu wa kawaida walikuwa wamezuiwa kulipata Neno la Mungu. Tyndale alikuwa amalizie kazi ya Wycliffe kwa kuwapatia watu wake Biblia. TK 159.2

Bila hofu yoyote alihubiri kile alichokuwa anakiamini. Tyndale alilijibu dai la Kanisa Katoliki kwamba lilikuwa limetoa Biblia na kuwa kanisa peke yake ndilo lililokuwa linaweza kifafanua Biblia kwa kusema: “Si kweli kwamba ninyi ndiyo mliotupatia Maandiko; ninyi ndiyo mliokuwa mmeyaficha Maandiko kwa ajili yetu; ninyi ndiyo mnaowachoma moto wale wanaoyafundisha, na kama mngeweza, mngekuwa mmeyachoma Maandiko.” 155 TK 159.3

Mahubiri ya Tyndale yaliamsha hamasa kubwa. Lakini mapadre walikuwa wanajaribu kuiharibu kazi yake. “Nini kifanyike?” kwa mshangao alitamka. “Siwezi kuwa kila mahali, Oh! Endapo Wakristo wangekuwa na Maandiko Matakatifu kwa lugha zao, wao wenyewe wangewakabili wapotoshaji hawa. Bila Biblia haitawezekana kuwaimarisha watu wa kawaida kwenye ukweli.” 156 TK 159.4

Kusudio jipya liliingia moyoni mwake. “Injili haiwezi kunena kwa lugha ya Kiingereza miongoni mwetu? Inalipasa kanisa kuwa na nuru kidogo wakati mchana kuliko wakati wa mapambazuko?... Ni lazima Wakristo walisome Agano Jipya kwa lugha ya kwanza.” 157 Ni kwa njia ya Biblia peke yake watu watauelewa ukweli. TK 160.1

Mkatoliki msomi aliyekuwa akibishana naye alitamka kwa mshangao, “Tulikuwa watu bora bila sheria za Mungu kuliko bila kuwa na sheria za Papa.” Tyndale alimjibu, “Ninamdharau Papa na sheria zake zote; na endapo Mungu atatunza maisha yangu, kabla ya miaka mingi nitamfanya mvulana anayelima kwa kutumia plau kujua zaidi Maandiko kuliko ninyi.” 158 TK 160.2