Tumaini Kuu

57/254

Sura Ya 10 - MAENDELEO NCHINI UJERUMANI

Kutoweka kwa Luther kwa njia zisizoeleweka, kulichochea hofu na mshangao mkubwa kote nchini Ujerumani. Uvumi mbaya ulisambazwa na wengi waliamini kuwa alikuwa ameuawa. Kulikuwa na maombolezo makubwa, wengi walinuia kwa kiapo cha pekee kulipiza kisasi kwa kifo chake. TK 120.1

Ingawa mwanzoni walishangilia sana uvumi wa kifo chake, maadui wa Luther waliingiwa na hofu kwamba alikuwa mateka. Mmoja wao alisema, “Njia pekee iliyobakia kwa ajili ya kupona kwetu ni kuwasha myenge, na kumsaka Luther popote alipo duniani, na kumrejesha katika taifa linalomhitaji.” 106 Habari ya kwamba alikuwa salama ingawaje alikuwa mfungwa ziliwafanya watu watulie, wakati huo huo Maandiko yake yakisomwa kwa shauku kubwa kuliko hapo kabla. Wengi walijiunga katika njia ya shujaa huyu aliyekuwa akililinda Neno la Mungu. TK 120.2

Mbegu alizokuwa amezipanda Luther zilichipuka kila mahali. Kutokuwepo kwake kulikamilisha kazi ambayo angekuwepo asingeweza kuifanya. Kwa kuwa kiongozi wao mkubwa alikuwa ameondolewa, watenda kazi wengine walisonga mbele ili kazi iliyokuwa imeanza vizuri isikwamishwe. TK 120.3

Shetani alianza kuwapotosha na kutaka kuwaangamiza watu kwa kuwashawishi kuamini maneno yasiyo kweli kwa kuwapatia kitu bandia mahali pa kazi ya kweli. Kama kulivyokuwa na makristo wa uongo kame ya kwanza, walitokea pia makristo wa uongo kwenye kame ya kumi na sita. TK 120.4

Watu wachache walijidhania kupokea ufunuo maalum kutoka mbinguni na kudai kuwa walikuwa wametumwa na Mungu kuendeleza Matengenezo, ambayo walidai, yalikuwa yameanzishwa kwa uhafifu na Luther. Lakini kwa kweli walikuwa wakiiharibu kazi aliyokuwa ameifanya. Waliikataa kanuni ya Matengenezo-kwamba Neno la Mungu lilikuwa linajitosheleza kabisa kama kanuni ya imani na matendo. Mwongozo usiokosea waliubadili kwa viwango vyao vya hisia na maono yasiyoaminika. TK 120.5

Wengine waligeuka kwa urahisi na kujiunga na watu hawa wenye itikadi kali ya kidini. Shughuli za mashabiki zilileta msisimko mkubwa. Luther alikuwa amewaamsha watu kuona hitaji la matengenezo, na kwa wakati huu watu waliokuwa waaminifu walipotoshwa na hawa “manabii wapya wa kujifanya.” Viongozi wa kundi hili walikwenda Wittemberg na kupeleka madai yao kwa Melanchthon: “Tumetumwa na Mungu kuwafundisha watu. Tumefanya mazungumzo ya karibu sana na Bwana; tunafahamu kile kitakachotokea; kwa kifupi, sisi ni mitume na manabii, na tuna maombi yetu kwa Dk. Luther.” TK 121.1

Wanamatengenezo walichanganyikiwa. Melanchthon alisema, ” Kuna roho asiye wa kawaida ndani ya watu hawa; lakini ni roho gani huyo?...Kwa upande mmoja, tunapaswa kuwa waangalifu tusije tukamzimisha Roho wa Mungu, na kwa upande mwingine tusije tukapotoshwa na roho wa Shetani.” 107 TK 121.2