Tumaini Kuu

11/254

Siku za Hatari kwa Kanisa

Wabeba bendera waaminifu walikuwa wachache. Wakati fulani, ilionekana kana kwamba uovu ungetawala kabisa, na dini ya kweli ingetokomezwa duniani. Injili ilikuwa haionekani, na watu walibebeshwa masharti magumu. Walifundishwa kutegemea matendo yao wenyewe kwa ajili ya upatanisho wa dhambi. Hija ndefu, malipizi, ibada ya vitu vilivyokuwa vinaheshimiwa na vilivyokuwa vinakumbushia mambo ya kale, kuinua makanisa, mahali patakatifu, na madhabahu, malipo ya kiasi kikubwa cha pesa kwa kanisa—haya yaliamriwa ili kutuliza ghadhabu ya Mungu au kukubalika mbele zake. TK 39.1

Ilipokaribia mwisho wa karae ya nane, utawala wa Papa ukatangaza kuwa katika miaka ya awali ya kanisa, maaskofu wa Kanisa la Roma walikuwa na uwezo wa kiroho kama ule waliokuwa wameanza kuwa nao sasa. Maandiko ya kale yakaghushiwa na watawa. Yakagunduliwa mabaraza ambayo yalikuwa hayajawahi kusikika huo nyuma, ambayo yalikuwa yanathibitisha ukuu wa Papa tangu mwanzo kabisa. (Angalia Kiambatisho). TK 39.2

Wajenzi wachache waaminifu waliojenga kwenye msingi imara (lKor.3:10, 11) walikuwa wanafadhaika. Wakiwa wamechoshwa na mahangaiko yasiyokoma dhidi ya mateso, ulaghai na kila kizuizi ambacho Shetani alikuwa anabuni, baadhi ya wale waliokuwa waaminifu walivunjika mioyo. Kwa sababu ya kutaka amani na usalama wa mali zao na maisha yao, waliuacha msingi ulio imara. Wengine hawakutishwa na upinzani wa maadui. TK 39.3

Ibada ya sanamu ikawa jambo la kawaida. Mishumaa ikawa inawashwa mbele ya sanamu na sala zikawa zinatolewa kwa sanamu hizo. Desturi za kipuuzi zikashamiri. Akili ikaonekana kana kwamba imepoteza udhibiti wake. Huku mapadri na maaskofu wenyewe wakiwa wapenda anasa na mafisadi, watu waliokuwa wakitegemea uongozi wao walitumbukizwa katika ujinga na uovu. Katika kame ya kumi na moja, Papa Gregori VII alitangaza kuwa kanisa lilikuwa halijawahi kufanya makosa, na lisingeweza kukosea, kulingana na Maandiko. Lakini dai hilo halikuambatana na ushahidi wa Maandiko. Askofu huyu mkuu mwenye kiburi, wa Kanisa la Roma alidai pia kuwa alikuwa na uwezo wa kuwaondoa madarakani wafalme. Kielelezo cha tabia hii ya ukatili ya huyu mtetezi wa dhana ya kutokosea kilikuwa jinsi alivyomtendea mfalme Henry IV wa Ujerumani. Mfalme huyu alipodiriki kudharau mamlaka ya Papa, alitengwa na kung’olewa kwenye kiti cha enzi. Wakuu wake wa majimbo walichochewa na mamlaka ya Papa wamwasi. TK 39.4

Henry IV aliona ulazima wa kupatana na Kanisa la Roma. Akiwa na mkewe na mtumishi wake mwaminifu alivuka milima ya Alps katikati ya kipupwe, ili aende kunyenyekea mbele ya Papa. Alipofika kwenye jumba la Gregory, alipelekwa kwenye ua wa nje. Akiwa huko alikaa kwenye baridi kali ya kipupwe, akiwa kichwa wazi na miguu pekupeku, akisubiri ruhusa toka kwa Papa ili aingie kumwona. Papa hakumsamehe mpaka alipoendelea kufunga na kuungama kwa siku tatu. Hata msamaha huo ulikuwa kwa sharti kwamba asubiri kibali cha Papa kuirudia taji yake au kutumia mamlaka ya kifalme. Gregory, akiwa amefurahishwa na ushindi wake, alijivuna akisema kuwa kushusha viburi vya wafalme, ulikuwa ni wajibu wake. TK 40.1

Kuna tofauti kubwa kati ya askofu huyu mwenye kiburi na Kristo, anayejieleza kuwa amesimama katika mlango wa moyo akisihi apate kuingia. Aliwafundisha wanafunzi wake kuwa: “na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu.” Mt. 20:27. TK 40.2