Tumaini Kuu

1/254

Tumaini Kuu

Kwa Nini Huna Budi Kusoma Kitabu Hiki

Kwa mamilioni ya watu, maisha ni kama jambo lisilo na maana wala mantiki. Sayansi, teknolojia, hata falsafa na teolojia, huwachukulia watu kama viumbe waliotokea kwa kudra. Lakini watu, wakijua au bila kujua, wameshindwa kukubaliana na maisha yasiyokuwa na malengo. Ghasia, upinzani na uasi, kujaribisha madawa ya kulevya—mambo haya kwa sehemu kubwa, ni namna ya watu kuonesha kuwa wanahangaika katika upotevu wao mkubwa. TK 11.1

Wanalia katika upweke na kukata tamaa kama watoto waliotawanyika kwa sababu ya vita, “Mimi ni nani? Wazazi wangu walikuwa akina nani? Ninawezaje kuwapata?” Wengi tunaigeukia sayansi ili tupate majibu, tukitegesha darubini zetu kubwa zitumiazo mionzi, kutazama mwenendo wa nyota kana kwamba tunauliza, “Kuna mtu ye yote anayenijua huko? Ni nani anayenijali? Lakini sayansi haina jibu. Sayansi ipo kwa ajili ya kuuliza maswali: Atomu imeundwaje, Inawezaje kugawanyika? Akili zetu zinafanyaje kazi? Ulimwengu wetu umeumbwaje? TK 11.2

Sayansi haiwezi kutwambia kwa nini kuna atomu, kwa nini wanadamu wapo, kwa nini ulimwengu upo. Wala haiwezi kujibu maswali ya pekee yanayowasumbua wanazuoni:Kama kuna kusudi jema na haki ulimwenguni, kwa nini waatu wema huteseka pamoja na waovu? TK 11.3

Je, kuna uhai baada ya kifo? Je, haiba ya mtu huwa inaendelea kuishi? Makanisa ya leo ya Kikristo yanamwakilisha Mungu? Ukweli ni nini? TK 11.4

Mustakabali wa ulimwengu ukoje? Je, utakoma huku ukilialia kama mtoto anayehangaika kuvuta hewa ya mwisho katika hali ya hewa iliyochafuka, au kwa mlipuko wa jehanamu utakatokana na makombora? Au, wanadamu-ambao katika historia hawajaweza kuonesha uwezo wa kuudhibiti ubinafsi wao-wataweza ghafla kukomesha uovu, vita, umaskini na hata mauti? TK 11.5

Kitabu hiki kinatoa majibu, tena ya kututoa wasiwasi. Uhai una makusudi! Hatuko peke yetu ulimwenguni. Kuna anayejali mahali fulani! Yupo kweli, aliyejihusisha na historia ya wanadamu, yeye aliyejiunga na jamii yetu, ili tuweze kumfikia na yeye aweze kutufikia yeye ambaye mkono wake wenye nguvu umekuwa juu ya sayari hii na ambaye ataiongoza kurudi kwenye amani-tena upesi. TK 11.6

Lakini miaka mingi iliyopita, kiumbe mmoja mlaghai ulimwenguni aliazimu kuitawala dunia yetu na kuuharibu mpango wa Mungu kwa ajili ya furaha ya familia yake ya duniani. Mwandishi wa kitabu hiki, ametumia lugha ya vielelezo—ambayo maelfu ya watu wameiita lugha iliyovuviwa—anafunua mambo yaliyokuwa hayajulikani sana na kuianika wazi mikakati ya kiumbe huyu mwenye nguvu, asiyeonekana, ambaye mikono yake iko tayari kuitawala wa dunia yetu. Kwa upande wa wanadamu, watawala wa kipagani pamoja na taasisi za kidini wanadhihirishwa kuwa washirika walio na hatia katika njama hizo. TK 12.1

Kitabu hiki kingeweza kuchapwa na kusambazwa katika kipindi chenye uhuru wa kidini tu, kwani kinazianika baadhi ya taasisi zenye nguvu kabisa katika siku zetu. Kinaeleza kwa nini matengenezo yalihitajika, na kwa nini yalisimamishwa; kisa cha makanisa yaliyoasi, juu ya ushirika wa watesi, muungano unaojitokeza wa kanisa na serikali ambao utafanya sehemu yake ya kidhalili kabla pambano kuu kati ya wema na uovu halijaisha. Katika pambano hili kila mwanadamu anahusika. TK 12.2

Mwandishi huyu anaandika hapa kuhusu mambo yaliyokuwa hayapo wakati wa uhai wake. Anaeleza kwa uaminifu usio wa kawaida. Masuala ya pambano ni makubwa na matokeo yake ni nyeti sana kiasi kwamba ilipasa mtu fulani atoe maneno haya ya kuonya na kuelimisha. TK 12.3

Hakuna mtu atakayefiingua kurasa za kitabu hiki kisha akakiweka bila kujiuliza kama haikuwa bahati kukiona. TK 12.4

Wachapaji