Kutayarisha Njia
Heri Kuvunja Uchumba Usio wa Busara
Kwa Kristo peke yake ndipo ushirika wa ndoa unamoweza kufungwa kwa usalama. Upendo wa mwanadamu ungefungamanishwa na upendo utokao mbinguni. Mahali Kristo anapotawala ndipo tu panapoweza kuonekana upendo wa kweli, usio wa hila wala kujipenda nafsi. KN 142.3
Hata kama uchumba umefanywa na mtu ambaye huelewi vyema tabia yake, usidhani kuwa kushika uchumba kutakulazimisha kutwaa kiapo cha ndoa, na kukuunganisha na mtu ambaye humpendi tena ambaye hutamheshimu maishani mwako, jihadhari sana unapofanya uchumba wenye masharti; lakini hata ikiwa ni uchumba wenye masharti, ni bora zaidi kuvunjilia mbali uchumba kama huo kabla ya kufunga ndoa kuliko kuja kuvunja ndoa baadaye, kama wengi wafanywavyo. Pengine utasema, “Lakini nimetoa ahadi yangu, je, niitangue? Mimi najibu, kama umekwisha kutoa ahadi kinyume cha Maandiko Matakatifu, kwa hali iwayo yote, itangue, bila kuchelewa, na kwa unyenyekevu mbele za Mungu tubu juu ya kupumbazika kwako ambako kulikufanya uharakishe kutoa ahadi kwa kiapo. Afadhali zaidi kuitangua ahadi ya namna hiyo, kwa kicho cha Mungu, kuliko kuitimiza, na kumdharau Mwumbaji wako. Kila hatua ihusuyo ndoa na iwe yenye adabu, unyofu, uaminifu, na kusudi jema la kumpendeza na kumheshimu Mungu. Ndoa huwa na matokeo ya baadaye katika ulimwengu huu na kwenye ulimwengu ujao pia. Mkristo mwaminifu hatafanya mipango ambayo haitampendeza Mungu. KN 142.4
Moyo unaoonea shauku upendo wa kibinadamu, lakini upendo huu sio wenye nguvu ya kutosha, au usafi wa kutosha, au tnamani ya kutosha kuwa badala ya upendo wa Yesu. Katika Mwokozi wake tu ndipo mahali mke awezapo kupata hekima, nguvu, na neema kuyakabili masumbufu, kazi, na taabu za maisha. Apaswa amfanye (Mwokozi) kuwa nguvu zake na kiongozi wake. Hebu mwanamke ajitoe kwa Kristo kabla ya kujitoa kwa rafiki awaye yote wa duniani, wala asiingie kwenye hali itakayokuwa kinyume cha hayo. Wale watakaoweza kupata furaha ya kweli hawana budi kuwa na mbaraka wa Mungu juu ya vyote walivyo navyo na juu ya mambo yote watendayo. Kutomtii Mungu ndiyo asili ya hali mbaya iliyo kwa wingi mioyoni na nyumbani mwa watu wengi. Dada yangu, kama usipoweza kupata nyumba isiyokuwa na hitilafu hata kidogo, usiungane na mtu aliye adui wa Mungu. KN 143.1