Kutayarisha Njia
Wapende Watu Wote
Tunaposikiliza lawama juu ya ndugu yetu, twajitwika lawama hiyo. Kwa swali hili, “Bwana, ni nam atakayekaa katika hema yako? Ni nani atakayefanya maskani yake katika kilima chako kitakatifu?” Mwandisni wa Zaburi amejibu, “Ni mtu aendaye kwa ukamilifu, na kutenda haki. Asemaye kweli kwa moyo wake, Wala hakumtenda mwenziwe mabaya, wala hakumsengenya jirani yake,” (Zaburi 15:1-3). KN 197.3
Mazungumzo hafifu yangezuilika kama nini ikiwa kila mtu angekumbuka kuwa wale wanaomwambia makosa ya wengine watatangaza makosa yake mara wakipata nafasi nzuri. Yafaa tujitahidi kuona mema kwa watu wote, hasa ndugu zetu, mpaka itakapotubidi kufikiri vinginevyo. Haitupasi kusifu upesi habari mbaya. Hizi mara nyingi hutokana na wivu na kutosikia vema, au pengine zimetiwa chumvi ama kutoa sehemu tu ya mambo ya kweli. Mara wivu na shuku vinapopewa nafasi, vitajieneza kama baruti. Kama ndugu akipotoka, huo ndio wakati wa kumwonyesha moyo wako hasa kwake. Mwendee kwa upendo, mwombee kwa Mungu ukiwa pamoja naye, kumbuka thamani isiyopimika ambayo Kristo amelipia ukombozi wake. Kwa njia hii waweza kuiokoa roho ya mtu na mauti, na kusetiri wingi wa dhambi. KN 197.4
Kutupia jicho, kutaja neno, hata kusema kwa sauti ya kuimba, huweza kujaa uongo wenye kupenya kama mshale wenye neno moyoni, utiao jeraha lisiloponyeka. Hivyo ndivyo mashaka, na lawama ziwezavyo kutupiwa mtu ambaye kwake Mungu angeweza kufanya kazi njema, na mvuto wake huharibiwa, na manufaa yake huangamizwa. Miongoni mwa wanyama wa aina nyingi, kama mmoja wao akijeruhiwa na kuanguka, mara hiyo hushambuliwa na kuraruliwa na wenzake. Moyo huo huo wa kinyama huonyeshwa na wanaume kwa wanawake wenye jina la Wakristo. Hao huonyesha moyo wa unafiki kuwapiga wengine mawe ambao ni wenye hatia pungufu kuliko waliyo nayo wao wenyewe. Kuna wengine ambao nuelekeza kwa kidole kwenye makosa ya wengine ili kuepusha hali yao wenyewe kutazamwa na watu, au ili kupata sifa kwa ajili ya moyo mkuu kwa Mungu na kwa kanisa. 2 KN 198.1
Wakati unaotumiwa kwa kuyalaumu makusudi na matendo ya watumishi wa Kristo ingekuwa bora ukitumiwa kwa maombi. Mara nyingi ikiwa wale wanaolaumu wengine wangejua ukweli juu ya watu wanaowalaumu, wangekuwa na maoni kinyume cha hayo juu yao. Basi, lingekuwa jambo bora kama nini ikiwa badala ya kuwalaumu na kuwashutumu wengine, kila mmoja angesema; “Sina budi kutimiza wokovu wangu mwenyewe. Ikiwa nashirikiana na Mwenye kutaka sana kuiokoa roho yangu, yanipasa kujilinda kwa uangalifu. Sina budi kuachilia mbali uovu wote maishana mwangu. Sina budi niwe kiumbe kipya ndani ya Kristo. Sina budi kushinda kila kosa. Ndipo, badala ya kuwadhoofisha wale wanaoshindana na maovu, naweza kuwatia nguvu kwa maneno yanayosaidia.” 3 KN 198.2