Tumaini la Vizazi Vyote

282/307

Jinsi Haki Ilivyochangamana na Rehema

Rehema za Mungu zilidhihirika kwa wanadamu kwa njia ya Yesu; lakini rehema haziwezi kutangua haki. Sheria isingeweza kubadilika, lakini Mungu alijitoa kafara mwenyewe kwa njia ya Kristo kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. “Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake.” 2 Wakorintho 5:9. Sheria huhitaji maisha ya haki na tabia kamilifu, na haya yasingeweza kutolewa na mwanadamu. Lakini Kristo, kama mwanadamu, aliishi maisha matakatifu na kukuza tabia kamilifu. Hali hizi huzitoa kama karama ya bure kwa watu wote wanaompokea. Maisha yake yanasimama badala ya maisha ya wanadamu. Kwa hiyo hufutiwa makosa yao ya zamani. Zaidi ya hayo, Kristo huwajaza wanadamu kwa sifa za Mungu. Huumba tabia ya mwanadamu kwa mfano wa tabia ya Mungu. Hivyo “haki itokayo kwa sheria” hutimilika katika yeye aaminiye katika Kristo. Mungu anaweza kuwa “mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu.” Warumi 3:26. TVV 433.1

Lilikuwa kusudi la Shetani kutenganisha rehema kutoka katika kweli na haki. Lakini Kristo alionyesha kuwa katika mpango wa Mungu mambo hayo huungana pamoja; moja haliwezi kuwepo pasipo jingine. “Haki na amani zimebusiana.” Zaburi 85:10. TVV 433.2

Kwa maisha yake na kifo chake, Kristo alithibitisha kuwa haki ya Mungu haikuangamiza rehema zake, bali kwamba dhambi inaweza kusamehewa, na kwamba sheria ni ya haki, na inaweza kushikwa kikamilifu. Mashitaka ya Shetani yalikanushwa. TVV 433.3

Udanganyifu mwingine ulikuwa sasa uletwe. Shetani alidai kuwa kifo cha Kristo kilitangua sheria ya Baba. Kama ingaliwezekana kwa sheria kubadilishwa ama kutanguliwa basi kusingekuwa na haja ya Kristo kufa. Lakini kutangua sheria kungedumisha milele uasi na kuuweka ulimwengu chini ya mamlaka ya Shetani. Kwa kuwa sheria haibadiliki, Yesu aliinuliwa juu ya msalaba. Hata hivyo kwa njia ile Kristo aliyoimarishia sheria, Shetani aliitumia kuonyesha kuwa ni kufutwa kwa sheria. Hapa ndipo litakapotokea pambano kuu la mwisho kati ya Kristo na Shetani. TVV 433.4