Tumaini la Vizazi Vyote

108/307

Uvuli Mzito

Picha ilionekana kuwa ni safi, lakini mbele yake kulikuwa na uvuli mzito kabisa, ambao ulifahamiwa na Yesu peke yake. “Siku zitakuja ambazo, bwana arusi ataondolewa kutoka kwao, ndipo hapo watafunga.” Watakapomwona Bwana wao akisalitiwa na kusulibishwa, ndipo wanafunzi watalia na kufunga. TVV 149.4

Atakapotoka kaburini, huzuni yao itageuka kuwa furaha. Baada ya kupaa kwake kwenda mbinguni, ataendelea kukaa pamoja nao kwa njia ya Mfariji, yaani Roho Mtakatifu, hapo hawatalia tena. Shetani anapenda kuwakatisha tamaa na kuwaambia kuwa wamedanganyika kabisa. Lakini kwa njia ya imani, watatazama katika patakatifu pa mbinguni, ambapo Yesu anapowahudumia. Lazima wafungue mioyo yao kwa Roho Mtakatifu, na kufurahi kwa ajili ya kuwako kwake. Walakini siku za kujaribiwa zitakuja. Wakati ambao Kristo hatakuwako kimwili, nao watashindwa kumtambua Mfariji, hapa basi itawafaa kufunga. TVV 149.5

Maandiko Matakatifu huonyesha aina ya kufunga ambayo hutakiwa na Mungu; ni kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kuvunja kila nira.” “Je siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta masikini waliotupwa nyumbani kwako?” Isaya 58:6, 10. Hapa ndipo inapoonyeshwa kazi ya Kristo. TVV 150.1

Yesu akiendelea kuwajibu wanafunzi wa Yohana, alitoa mfano: “Hakuna mtu atiaye kiraka kipya kwa nguo kuukuu, maana kiraka hicho kitaipasua nguo.” Mathayo 9:16. Majaribio ya kuafikanisha mapokeo na ushirikina wa Mafarisayo pamoja na dini halisi ya Yohana kungethibitisha matengano makubwa zaidi. TVV 150.2

Wala kanuni za mafundisho ya Kristo zisingalipatana na dini ya nje ya Mafarisayo. Kristo angetofautisha wazi baina ya dini ya zamani na ile mpya.” Wala watu hawaweki divai mpya katika viriba vikuukuu, maana wakifanya hivyo viriba vitapasuka na divai itamwagika; lakini divai mpya huwekwa katika viriba vipya, vikahifadhika vyote. Mathayo 9:17. Viriba vilitumiwa kuwekea divai mpya, lakini baada ya wakati kupita, hukauka, na kupasuka, na hivyo huwa havifai kutumika tena. Viongozi wa wayahudi walikazana kushika mapokeo tu na ibada za nje nje, bali roho zilifanana na viriba vilivyokauka. Kwa vile walivyoridhika na dini yao, hawakutaka kuona mambo mapya yakiingizwa katika dini yao. Dini ya kweli, ifanyayo kazi kwa upendo, haikupata nafasi katika dini ya Mafarisayo. Hii hutakasa mioyo na kuipa uzima mpya. Mafarisayo walikuwa na dini ya mfano tu ya kanuni za wanadamu. Kuunganika na dini ya kweli ya Kristo ingekuwa kazi bure. Ukweli wa Mungu, usingaliingia katika viriba vya mapokeo ya Mafarisayo. TVV 150.3