Maranatha

42/183

Maswali ya Kujihoji, Sura ya 42

Ni nani atakayepanda katika mlima wa BWANA? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake? Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili, wala hakuapa kwa hila. Zaburi 24:3,4. Mar 50.1

Roho ambayo imeunganika na Kristo... itapigana dhidi ya kila ukosaji na kila mwonekano wa dhambi. Kila siku itaendelea kufanana na nuru ing’aayo kwa upevu, na pia kuupata ushindi zaidi. Roho hii itaendelea toka uwezo hadi uwezo, na siyo toka udhaifu hadi udhaifu. Mar 50.2

Hebu yeyote asijidanganye katika suala hili. Kama unalea kiburi, kujiinua nafsi, kupenda kukwezwa, kupenda makuu, tamaa ya mambo yasiyo matakatifu, manung’uniko, kutoridhika, ukali, kunena maovu, kuongopa, udanganyifu, uzushi, Kristo hakai ndani ya moyo wako.... Sharti uwe na tabia ya Kikristo ambayo itasimama kwa kudumu... Mar 50.3

Inapasa iwepo mijadala makini kati ya wale wanaodai kuiamini kweli, la sivyo wataanguka siku ya hukumu. Sharti watu wa Mungu wafikie kiwango cha juu. Wanapaswa wawe taifa takatifu, watu wa pekee, kizazi kilichoteuliwa - chenye ari ya kutenda matendo mema. Kristo hakufa kwa ajili yako ili upate kuwa na shauku, mionjo na mazoea ya watu wa ulimwengu. . . Mar 50.4

Hakuna mtu atakayepita katika malango ya utukufu bali yeye ambaye ameuelekeza moyo wake hivyo. Kisha, maswali kama haya yafuatayo, yanapata nafasi yake; je, unajali zaidi mambo ya kidunia? Je, mawazo yako ni safi? Je, unavuta hewa ya mbinguni? Je, unazunguka katika hewa mbaya iliyochafuka?. . Je, umejitoa na unayo bidii, ukimtumikia Mungu katika usafi na katika uzuri wa utakatifu wake? Jiulize kwa uaminifu, Je, mimi ni mtoto wa Mungu, au la?. . . Mar 50.5

Tunahitaji matengenezo ya dhati katika makanisa yetu yote. Nguvu ya Mungu inayoongoa sharti ije kanisani...Usiiahirishe siku ya maandalizi. Usisinzie ukiwa katika hali ya kutokuwa tayari, hali ya kutokuwa na mafuta katika vyombo vya taa zenu. . . Hebu swali lisisalie katika hali ya hatari na kutokuwa na hakika. Jiulize mwenyewe kwa udhati, Je, mimi nimo kati ya wanaookolewa, au wasiookolewa? Je, nitasimama au la? Yule tu mwenye mikono safi na moyo mweupe ndiye atakayesimama katika siku ile. Mar 50.6

Ni fursa ya pekee kwa kila mwana wa Mungu kuwa Mkristo wa kweli kila wakati; hapo anakuwa na kibali cha Mbingu kwa ajili yake. Mar 50.7