Maranatha

1/183

Maranatha

Kuja kwa Yesu Mara ya Kwanza, Sura ya 1

Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe..., kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. Wagalatia 4:4,5. Mar 9.1

Kuja kwa Mwokozi kulitabiriwa katika bustani ya Edeni. Adamu na Hawa walipoisikia ahadi hiyo kwa mara ya kwanza, walitazamia itimie upesi. Walimpokea mtoto wao wa kwanza kwa furaha, wakitumaini kuwa angekuwa ndiye Mkombozi. Lakini utimilifu wa hiyo ahadi ulizidi kukawia. Wale walioipokea mara ya kwanza walikufa bila kuiona. Tangu siku za Henoko ahadi hiyo ilisimuliwa na wazee na manabii, wakilidumisha tumaini la kuonekana kwake, lakini bado hakuja. Unabii wa Danieli ulielezea muda wa kuja kwake, lakini si wote walioufasiri ujumbe huo kwa usahihi. Karne ziliendelea kupita; sauti za manabii zikakoma. Mkono wa mtesi ukawaelemea wana wa Israeli, na wengi walikuwa wanakaribia kusema, “Siku hizo zinakawia na maono yote hayatimizwi.” Eze. 12:22. Mar 9.2

Lakini kama vile nyota zinavyopita katika njia zilizopangiwa, makusudi ya Mungu hayawezi kuharakishwa wala kuchelewa. Mungu alikuwa amemwonesha Ibrahimu utumwa wa Israeli kule Misri kwa njia ya giza kuu na tanuru lililokuwa linafuka moshi, na alikuwa amesema kuwa utumwa wao ungedumu kwa miaka mia nne. Alisema, “Baadaye watatoka na mali mengi.” Mwa. 15:14. Nguvu zote za ufalme wenye kiburi wa Farao zilipambana na neno hilo bila mafanikio. “I likuwa siku ile ile” iliyotajwa katika ahadi ya Mungu, “ya kwamba majeshi yote ya Bwana yalitoka nchi ya Misri.” Kut. 12:41. Hivyo ndivyo saa ya kuja kwa Kristo ilivyokuwa imepangwa katika baraza la mbinguni. Saa ilipoonesha kuwa muda huo umefika, Yesu alizaliwa kule Bethlehemu. Mar 9.3

“Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe.” Mungu alikuwa amepangilia mwenendo wa mataifa, na mwelekeo wa msukumo na mvuto wa wanadamu, mpaka ulimwengu ulipokuwa tayari kwa ajili ya ujio wa Mkombozi. . . Mar 9.4

Wakati huo Yesu alikuja kurejesha sura ya Mwumbaji kwa wanadamu. Hakuna mtu zaidi ya Kristo anayeweza kufanya upya tabia ambayo imeharibiwa na dhambi. Alikuja kutoa pepo wabaya ambao walikuwa wanatawala mapenzi ya wanadamu. Alikuja kutuinua kutoka mavumbini, kuiunda upya tabia ili ifanane na tabia ya Mungu, na kuifanya ipendeze kwa utukufu wake mwenyewe. Mar 9.5