Kumjua Yesu
KUMJUA YESU
YALIYOMO
Sura 1—Jinsi Mungu Anavyowapenda Wanadamu
VIUMBE vya ulimwengu, na jinsi Mungu alivyowafunulia wanadamu mambo yajayo, vyote huonyesha upendo wa Mungu. Baba yetu aliye mbinguni ndiye asili ya uhai, hekima, na furaha. Vitazame viumbe vyote jinsi vilivyo vizuri na vya ajabu. Fikiri jinsi vifaavyo kwa mahitaji na furaha, siyo ya wanadamu tu, bali ya viumbe vyote vilivyo hai. Jua na mvua, vinavyofurahisha na kuburudisha nchi, pamoja na vilima, bahari na mabonde, vyote hutuonyesha upendo wa Muumba wetu. Mungu ndiye anayeviruzuku viumbe vyake vyote mahitaji yao ya kila siku. Katika maneno mazuri ya Mtunga Zaburi twasoma haya,— KY 7.1
“Macho yao wote yakutazamia wewe;
Nawe huwapa chakula chao majira yake.
Hufunua mkono wako,
Humshibisha kila hai uradhi.” Zaburi 145:15, 16.
KY 7.2
Mungu alimwumba mwanadamu katika hali ya furaha na utakatifu kamili; na wakati nchi ilipotoka mkononi mwa Muumba, ilikuwa nzuri kabisa; haikuwa na dalili ya uharibifu wala ya laana ya Mungu. Taabu na mauti viliingia kwa ajili ya kuharibu amri za Mungu. Walakini upendo wa Mungu huonyeshwa hata kwa maumivu yaliyokuja kwa ajili ya dhambi. Imeandikwa kwamba Mungu aliilaani ardhi kwa ajili ya mwanadamu. Mwanzo 3:17. Miti yenye miiba na magugu—yaani shida na majaribu yanayompata mwanadamu katika uzima wake—yaliwekwa kuwa msaada wake, kuwa ni namna mojawapo ya mafundisho yake yanayotakiwa katika mpango wa Mungu juu ya mwanadamu, ili apate kumtoa katika hali mbaya ya dhambi na kumrudisha katika hali njema jinsi alivyokuwa mara ya kwanza. KY 7.3
Ingawa dunia imeanguka katika hali mbaya kwa ajili ya dhambi, lakini yote yaliyomo si huzuni na mashaka. Viumbe vimekuwa kama mitume wa Mungu kutuletea maneno ya kututia faraja na kututuliza roho zetu. Kila mti wa miiba una maua yake; yaani, katika kila shida twaweza kupata baraka za Mungu. KY 8.1
“Mungu ni pendo” imeandikwa kila mahali. Ndege waimbao vizuri, kila aina ya maua na miti,—yote hutushuhudia upendo na uangalifu wa Mungu, jinsi atakavyo kuwafurahisha watoto wake. KY 8.2
Neno la Mungu huonyesha tabia zake. Yeye mwenyewe ametangaza upendo wake na huruma yake visivyo na kiasi. Musa alipoomba, “Nionyeshe basi utukufu wako,” Bwana alimjibu akanena, “Nitapitisha mimi wema wangu wote mbele yako.” Huu ndio utukufu wake. Bwana alipita mbele ya Musa, akatamka, “Bwana, Bwana Mungu, mwenye rehema na neema, si mwepesi kwa hasira, na mwingi wa huruma na kweli; awawekeaye elfu huruma, mwenye kusamehe uovu, na kosa, na dhambi.” Kutoka 33: 18,19; 34: 6, 7. Naye “mvumilivu, na mwenye wema mwingi,” “kwa sababu apendezwa na huruma huyu.” Yona 4: 2; Mika 7:18. KY 8.3
Mungu amejifungia mioyo yetu kwake kwa namna nyingi zinazotuonyesha upendo wake; katika viumbe vya ulimwengu, na kwa upendano ulio wema wa wanadamu, Mungu amejaribu kutuonyesha wema wake. Lakini hayo yote hayawezi kutudhihirishia barabara upendo wake jinsi ulivyo, kwa kuwa adui, yaani Shetani, amepofusha macho va kiroho ya wanadamu ili wawe na hofu kwa Mungu; nao humwona Mungu kama ni mkali asiye na huruma. Shetani aliwapoteza wanadamu ili wamdhanie Mungu kuwa ni mkali kabisa—kama mwamuzi aliye na roho ngumu asiyeweza kumwachia mtu. Aliwatilia wanadamu fikara kama Muumba wetu huwachunguachungua watu ili apate kujua makosa yao na kuwalipiza kisasi. Bwana Yesu alikuja hapa duniani na kuishi kati ya wanadamu kwa kusudi kuziondolea mbali fikara mbaya hizo, na kutuonyesha upendo wa Mungn jinsi ulivyo. KY 9.1
Mwana wa Mungu alitoka mbinguni ili awaonyeshe wanadamu Baba aliye mbinguni. “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mwana wa pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyefasiri habari yake.” “Wala hakuna mtu amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.” Yoh. 1:18; Mattayo 11:27. Mmoja wa wanafunzi wake alipomwambia, “Tuonyeshe Baba,” Yesu alimjibu, “Nimekuwa pamoja nanyi siku hizi zote wala hukunijua, Filipo? Aliyeniona mimi, amemwona Baba; wasemaje wewe, Tuonyeshe Baba?” Yoh. 14:8, 9. KY 10.1
Yesu alipoeleza namna ya kazi yake aliyojilia kuifanva hapa duniani, alisema hivi,— KY 10.2
“Roho ya Bwana ni juu yangu,
Kwa sababu amenitia mafuta kuwahubiri
maskini habari njema.
Amenituma kuwaponya waliopondeka moyo,
Kuwatangazia wafungwa kufunguliwa,
na vipofu kupata kuona tena,
Kuwaacha huru waliosetwa.” Luka 4:18.
KY 10.3
Hiyo ndiyo kazi yake. “Naye akatembea huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Shetani.” Matendo 10:38. Katika matendo yake yote alionyesha upendo, rehema na huruma. Alikuwa katika hali ya kibinadamu ili apate kujua mahitaji ya wanadamu. Hakuna hata maskini kabisa aliyeogopa kumfikilia karibu. Watoto pia wakavutwa kwake. KY 10.4
Yesu hakuficha neno lo lote la kweli, lakini aliyesema yote katika moyo wa upendo. Alitumia busara sana na uangalifu na huruma katika maongezi yake na watu. Hakuwafanyia watu jeuri kamwe, hakusema maneno yo yote makali yasipohusu, hakuwahuzunisha watu bila maana. Hakuulaumu udhaifu wa kibi¬nadamu. Alisema kweli tupu, lakini alisema yote katika moyo wa upendo. Alichukizwa sana na hali ya unafiki, na kutokuamini, na uovu; lakini kila aliposema maneno ya lawama na mashtaka, aliyesema kwa masikitiko makubwa. Aliulilia Yerusalemi, mji alioupenda, ambao ulikataa kumpokea yeye aliye Njia, Kweli, na Uzima. Walimkana yeye aliye Mwokozi, lakini hata hivyo akazidi kuwahurumia. Maisha yake yalikuwa ya kujinyima mwenyewe na kuwafikiria wengine. Kila mtu alikuwa na thamani kubwa machoni pake. Ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, hakumdharau mwanadamu ye yote; bali aliwaona wote kuwa ni wenye dhambi ambao alikuja kuwaokoa. KY 11.1
Hizo ndizo tabia zake Kristo kama zilivyofunuliwa katika maisha yake. Tena hizo ndizo tabia za Mungu mwenyewe pia. Yesu, Mwokozi aliye mwema, mwenye huruma, ndiye Mungu hasa aliyedhihirishwa katika mwili wa kibinadamu. 1 Tim. 3:16. KY 11.2
Yesu aliishi, akateswa, akafa ili atukomboe. Alikuwa “mtu wa huzuni,” ili tuwe washiriki pamoja naye katika furaha ya milele. Naye Mwana Mpendwa wa Mungu, aliyejaa neema na kweli, Mungu alimwacha atoke mahali pa utukufu na kufika hapa duniani, palipoharibika kwa ajili ya dhambi, penye giza ya mauti na laana. Alimkubalia atoke mahali anapopendwa na Babaye na kusifiwa na malaika, aje kuaibika, kudhiliwa, kuchukiwa, na kuuawa. “Adhabu ya amani yetu juu yake.” Isa. 53: 5. Mwangalie jinsi alivyo jangwani, katika bustani ya Gethsemane, tena juu ya msalaba. Mwana Mtakatifu wa Mungu akachukua mwenyewe uzito wa dhambi ya wanadamu. Yeye aliyekuwa na umoja na Mungu, akaona mwenyewe moyoni mwake ubaya wa hali ya kutengana na Mungu, ndiyo hali ya wanadamu kwa ajili ya dhambi. Kwa ajili ya matengano hayo akaona uchungu moyoni naye akalia, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Mattayo 27:46. Uzito wa dhambi, jinsi ulivyo mbaya kupita kiasi, na jinsi unavyoleta kutengana na Mungu—huu ndio uliouvunja moyo wa Mwana wa Mungu. KY 12.1
Lakini Yesu hakujitoa kuwa dhabihu kubwa hivi makusudi kumtilia Baba yake moyo wa kuwapenda wanadamu na kuwaokoa. Sivyo! “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akampeleka Mwana wake wa pekee, ili mtu aliye yote amwaminiye asipotee, bali apate uzima wa milele.” Yoh. 3:16. Tangu zamani Baba yetu aliye mbinguni ametupenda, si kwa ajili ya upatanisho alioufanya Yesu, ila kwa kuwa Mungu mwenyewe alitupenda, naye akamkubali Yesu afanye upatanisho huo. Kristo ndiye njia ambayo kwayo Mungu hutuonyesha upendo wake kwetu. “Yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake.” 2 Wakor. 5:19. Mungu alipata maumivu pamoja na Mwanawe. Huko Gethsemane, na kwa kufa kwake Kalwari, Mungu alijitoa kwa ajili ya wokovu wetu. KY 12.2
Yesu alisema, “Ndio maana Baba anipenda, kwa sababu nauweka uzima wangu ili niutwae tena.’ Yoh. 10:17. Yaani, ni kama Yesu angesema hivi: “Baba yangu amewapendeni sana hata anazidi kunipenda mimi kwa sababu ya kujitoa maisha yangu kwa ajili yenu. Mimi nikawa ninajitoa badala yenu tena kuwa kama dhamana yenu, na kwa jinsi nilivyochukua makosa yenu na adhabu ambayo iliwapasa ninyi, kwa hayo Baba yangu huzidi kunipenda mimi; kwa sababu ya Dhabihu yangu, Mungu aweza kuwa mwenye haki tena kumhesabia haki yule amsadikiye Yesu.” KY 13.1
Hakuna awezaye kutuokoa, ila Mwana wa Mungu tu; kwa kuwa yeye pekee aliyekuwa pamoja na Baba, ndiye awezaye kumsifu na kueleza tabia zake. Yeye tu aliyeujua upendo wa Mungu ndiye awezaye kuudhihirisha upendo ule barabara. Hakuna njia nyingine ya kutuonyesha jinsi Mungu anavyowapenda wanadamu waliopotea, ila kwa njia hii moja tu, yaani ya Kristo alivyojitoa na kufa badala yao. KY 14.1
“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akampeleka Mwana wake wa pekee.” Yoh. 3:16. Mungu alimtoa Mwanawe aishi kati ya wanadamu ili azichukue dhambi zao, apate kuadhibiwa badala yao, na kuwatolea maisha yake kama dhabihu; pia Mungu akamtoa awe katika hali moja na wanadamu ambao wamepotea, na kushirikiana nao katika mambo ya maisha yao na haja zao zote. Yeye aliyekuwa mamoja na Mungu amejiunga na wanadamu kwa namna isiyoweza kuvunjwa. Yesu “haoni haya kuwaita ndugu zake.” (Waeb. 2:11); yeye ndiye Dhabihu yetu, Mwombezi wetu mbele ya Mungu, Ndugu yetu aliye katika mfano wa kibinadamu na kushirikiana nao hao ambao amekuja kuwaokoa—Yeye ndiye Mwana wa mwanadamu. Alifanya hayo yote ili awakomboe wanadamu katika dhambi na hali yake mbaya, naye mwanadamu apate kujua upendo wake Mungu na kushirikiana naye katika hali ya furaha na usafi. KY 14.2
Tukifahamu kimo cha wokovu wetu, jinsi Mwana wa Mungu alivyokufa kwa ajili yetu, imetulazimu kutambua jinsi tunavyoweza kuwa watu walio bora katika Kristo. Mtume Yohana alipofahamu upendo wa Mungu jinsi ulivyo mkubwa mno, aliona hana budi kumcha Mungu na kumsujudu moyoni mwake. Upendo huo, jinsi ulivyo wa huruma na rehema, ni upendo mkubwa usioweza kusemeka; naye Yohana alisema, “Fahamuni, ni pendo la namna gani alilotupa Bwana, kuitwa wana wa Mungu.” 1 Yoh. 3:1. Mungu amewaona wanadamu kuwa ni wenye thamani kubwa ya namna gani! Kwa kuanguka katika kufanya dhambi, wanadamu wakawa chini ya mamlaka ya Shetani. Lakini kwa kumwamini Kristo na kutolewa kwake, waweza kuwa wana wa Mungu. Kristo alikuwa katika hali ya kibinadamu ili apate kuwasaidia wanadamu. Nao wenye dhambi wakiwa wanashirikiana naye Kristo, watageuzwa hali yao, na kustahili kuitwa “wana wa Mungu.” KY 15.1
Upendo wa ajabu huo, hauwezi kulinganishwa na kitu cho chote! Wana wa Mfalme aliye mbinguni! Ahadi ya kupendwa sana! Jambo la maana sana lifaalo kufikiriwa! Upendo usio na kifani, jinsi Mungu alivyoupenda ulimwengu usiompenda! Fikara hiyo huutiisha moyo na kuutuliza ili ufungwe kwake Mungu na kufanya mapenzi yake. Na jinsi tunavyozidi kuzichungua tabia za Mungu, na kufahamu jinsi alivyotufanyia kwa kufa kwake Kristo msalabani, ndivyo tunavyozidi kuona kama Mungu ndiye mwenye rehema na huruma, na ndiye awezaye kuwasamehe wenye makosa, naye ni mwenye haki, naye huwapenda wanadamu kwa upendo mkubwa upitao kiasi cha upendo wa mama kwa watoto wake. KY 15.2
Mapenzi ya milele
Ndiyo yanipendayo;
Yalinipenda mbele,
Sina fahamu nayo;
Sasa amani yake
Tele rohoni mwangu,
Ni mimi kuwa wake,
Na Yeye kuwa wangu.
Ni mimi kuwa wake,
Na Yeye kuwa wangu.
Wake hata milele,
Si kutengana tena;
Hunipa raha tele
Moyoni mwangu, Bwana
Hiyo nchi na mbingu
Zitatoweka zile;
Ni wake, Yeye mbwangu,
Milele na milele,
Ni wake, Yeye mbwangu,
Milele na milele.
KY 16.1